Mchome aivimbia CHADEMA kumvua uongozi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:02 PM May 17 2025
Lembrice Mchome
Picha: Mpigapicha Wetu
Lembrice Mchome

Lembrice Mchome, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Mwanga, aliyeng'olewa madarakani leo na Baraza la Mashauriano Mkoa wa Kilimanjaro, amesema anatambua kuwa yeye bado ni kiongozi halali wa chama wilayani humo.

Akizungumza na Nipashe Digital amesema: "Sijapokea barua yeyote, sijapokea taarifa yeyote, mimi ninachotambua bado ni kiongozi wa Wilaya ya Mwanga."

Mei 17 mwaka huu, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Ndonde Tottinan, ametangaza kuwa Mchome amevuliwa uongozi, baada ya kufanyika kikao cha baraza la mashauriano, mkoa wa Kilimanjaro.

Alipotafutwa kutoa ufafanuzi, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Ndonde Tottinan, amesema sababu ya kwanza ya kumuondoa, ni utekekezaji wa shughuli za chama kwa mujibu wa katiba ya chama hicho Ibara ya 6:3:4, ambayo inaeleza moja ya sababu ya uongozi unavyoweza kukoma, kuwa ni pamoja na kushindwa kutimiza wajibu wake.

"Sasa kwa sababu hayo yako kwenye ngazi ya jimbo, kamati ya uongozi inaelekeza kamati za utendaji ambazo zina jukumu la kufanya na kusimamia shughuli za chama. Katiba inasema kila baada ya miezi mitatu ni lazima kufanyika vikao vya kikatiba kwa maana ya kamati tendaji vinavyotanguliwa na vikao vya kila mwezi vya sekretarieti ya chama.

...Sasa tangu amechaguliwa mwaka jana mpaka leo, hakuna kikao chochote cha kamati tendaji kimekaa. Kwenye majukumu ya kamati tendaji, Ibara ya 7:4:10 imeeleza kwamba moja ya majukumu ya kamati tendaji, ni kuandaa mpango mkakati wa chama kwenye ngazi ya jimbo."

Ndonde, amesema mara kadhaa ofisi yake, akiwa kama Katibu Kanda ya Kaskazini, alimuandikia barua 25/3/2025 ya kutaka kupewa taarifa ya mihtasari ya vikao vilivyofanyika, lakini alitaka kujua mpango wa chama na ziara za chama, kwa maana ya ujenzi wa chama kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya.

Ameenda mbali zaidi akisema, ilipofika 12/4/2025 alikumbusha tena kwenye kikao cha Baraza la Mashauriano Mkoa wa Kilimanjaro, akiagiza kupata taarifa hizo lakini hakupata.

"Tarehe 17/4/2025 nikarudia tena kukumbushia utekelezaji, lakini mpaka sasa hatujawahi kupata utekelezaji wowote. Kwa hiyo hapo hakuna shughuli yeyote ya kichama inayofanyika Wilaya ya Mwanga.

"Kwa msingi huo, tumeamua tuvunje uongozi wa Wilaya ya Mwanga (Mwenyekiti), kwa sababu viongozi waliokuwepo wameshindwa kutekeleza majukumu yao."