Tabibu mbaroni kwa wizi vifaatiba vya Mil.28.5/-

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:53 PM May 17 2025
Tabibu mbaroni kwa wizi vifaatiba vya Mil.28.5/-
Picha: Mpigapicha Wetu
Tabibu mbaroni kwa wizi vifaatiba vya Mil.28.5/-

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, linawashikilia na kuwahoji watu wawili akiwemo Ofisa tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Nyanda Thomas (35) kwa tuhuma za wizi wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh.milioni 28.51.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kukamatwa kwa watu hao leo Mei 17, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema tabibu huyo ni mkazi wa mtaa wa Maduka Manane pamoja na mwenzake Novart Felician (36), mkazi wa mtaa wa Soweto, wilaya ya Sengerema.

Kamanda Mutafungwa amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kutekeleza wizi huo katika hospitali ya wilaya ya Sengerema Aprili 4, 2025 majira ya saa mbili asubuhi.

Ametaja vifaa vilivyoibiwa kuwa ni pamoja Fetal heart rate monitor 05, Central monitor system 01, Difibrillator 01, Infusion pump 02, Nebulizer machine 02, Syringe pump 02 na Blood pressure machine 04, vyote vikiwa na Sh.milioni 28.51.

Amesema baada ya tukio hilo kuripotiwa katika kituo cha Polisi, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi na kufanya msako  na kuwa Mei 15, 2025 majira ya saa nne asubuhi lilifanikiwa kuwatia mbaroni ofisa tabibu huyo pamoja na mwenzake ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa Chuo na kituo cha Afya kiitwacho ELABS, wakiwa na vifaa hivyo.

Kamanda Mutafungwa amesema, katika mahojiano ya awali mtuhumiwa Novert Felician alikiri kuwa aliuziwa vifaa hivyo na Nyanda Thomas ili avitumie katika kituo chake cha afya na chuo.  

Amesema Vifaa tiba vilivyokamatwa ni Difibrillator 01, Infusion pump 02, Nebulizer machine 02, Syringe pump 02, Blood pressure machine 04, Fetal heart rate monitor 03 na Central monitor system 01.

Amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo  ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wote walio husika katika kupanga na kushiriki katika wizi huo.

Amesema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.