Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro kimejaza kwa muda nafasi mbalimbali za uongozi kufuatia kujitoa uanachama kwa waliokuwa viongozi.
Waliojitoa unachama ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Gervas Mgonja, Katibu wa Mkoa Basil Lema, pamoja na viongozi wengine akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Grace Kiwelu.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi na makada wa CHADEMA kutoka Mkoa wa Kilimanjaro , Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Wakili Samwel Welwel amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Katiba ya chama chao ili kuhakikisha uongozi unaendelea bila pengo.
Aidha, Anna Mushi amekabidhiwa jukumu la kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa BAWACHA mkoani humo, na Irene Lema akikaimu nafasi ya Katibu wa Bawacha.
Kwa upande wake, Katibu wa Kanda, Ndonde Totinan, amesema uteuzi huo umezingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uadilifu, uaminifu na uwezo wa kiuongozi waliouonesha viongozi hao ndani ya chama kwa kipindi cha nyuma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED