WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Lindi, imetangaza kusitisha matumizi ya barabara ya Somanga-Mtama, kwa muda baada ya mvua kubwa zilizonesha katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Mvuoa hizo, zimeleta mafuriko makubwa yaliyoharibu eneo la barabara lililo kwenye njia ya mchepuko ya ujenzi wa daraja la Somanga-Mtama.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, amesema maji yamejaa katika eneo hilo na kusababisha barabara kutoweza kupitika kwa sasa.
“Mtendaji Mkuu amelekeza barabara hii ifungwe, ili kutoa nafasi ya kuchunguza hali ya uharibifu na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara. Tunawashauri wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zaidi kutoka mitandao ya kijamii ya TANROADS," alisema Mhandisi Zengo.
"Maji yatakapopungua, tutaanza kufanya kazi ya kurejesha mawasiliano na barabara itafunguliwa mara moja," ameongeza.
Mhandisi Zengo amesisitiza kuwa usalama wa watumiaji wa barabara ni kipaumbele cha kwanza, na hivyo kuwalazimu kuifunga barabara hiyo kwa muda.
Amesema wananchi wataendelea kupewa taarifa rasmi kila hatua kuhusu maendeleo ya hali hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED