EWURA kuendelea kuhamasisha matumizi nishati safi ya kupikia

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 06:25 PM Jul 06 2024
Baadhi ya wananchi wakiendelea kupata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendele katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Picha: EWURA
Baadhi ya wananchi wakiendelea kupata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendele katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha jamii kuhusu matumuzi ya nishati safi ya kupikia.

Lengo ni  kuendana na Mkakati wa Kitaifa ambao umelenga kuhakikisha Watanzania wanahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya mkaa.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya  Biashara (Sabasaba) yanayofanyika  barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Kaguo amesemaa kuwa serikali itaendelea pia kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika vyombo vya moto ikiwemo magari ili kuendeleza matumizi ya nishati safi huku wito ukitolewa kwa wawekezaji kujikita katika uwekezaji wa vituo vya gesi hiyo –CNG.

“Tunawahamasisha wawekezaji wawekeze kwenye vituo vya ujazaji wa gesi asilia ambapo utaratibu umesharekebishwa na TBS kwamba kituo cha mafuta kinaweza kuwa kinauza gesi asili kwenye magari,” amesema Kaguo.

Pamoja na mambo mengine Kaguo amesema EWURA imekusudia kutumia maonesho hayo katika kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinatolewa na mamlaka hiyo.

Amesema kupitia Maonesho hayo imekuwa fursa kukutana na wadau pamoja na wananchi kwa ujumla kutoa elimu kuhusu masuala ya petroli, umeme, gesi asilia pamoja na maji na usafi wa mazingira.