RC Macha ashuhudia utiaji saini mikataba matengenezo ya barabara ya sh.bilioni 10.2/-

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:56 PM Oct 05 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akishuhudia utiaji saini mikataba ya matengenezo ya barabara baina ya TARURA na Wakandarasi.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akishuhudia utiaji saini mikataba ya matengenezo ya barabara baina ya TARURA na Wakandarasi.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, ameshuhudia utiaji saini mikataba 33 ya matengenezo ya miundombinu ya barabara, baina ya wakandarasi na wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoani humo yenye thamani ya sh.bilioni 10.2.

Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo 33 imefanyika leo Oktoba 4,2024 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa shinyanga.

Macha akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo,amewataka wakandarasi, kwamba miradi hiyo waitekeleze kwa uzalendo,weledi na ubora unaotakiwa, ili kuendana na thamani ya fedha “value for money” na kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu.

Amesema barabara ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu katika shughuli zake mbalimbali ikiwamo na kukuza uchumi, na kuwasihi wakandarasi wajitume kufanya kazi,na kwamba katika utekelezaji wa miradi hiyo waitekeleze wenyewe kupitia makampuni yao, na siyo kwenda kuwapatia watu wengine ambao hawana uwezo na kuharibu kazi hiyo.


“Msiende kugawa kazi hizi kwa watu wengine,nendeni mkazifanye wenyewe kama milivyoomba kupitia makampuni yenu, tunataka barabara hizi na madaraja yatengenezwe kwa ubora unaotakiwa,na mimi nitakuwa nafanya ziara ya kuzikagua,”amesema Macha.

Aidha,amewataka pia wakandarasi kwamba wanapokuwa wakitekeleza miradi hiyo washirikishe wananchi wa maeneo husika, pamoja na kuwapatia ajira zisizo hitaji ujuzi mkubwa, kutoa mikataba sahihi na kuwalipa kwa wakati.

Amewasisitiza pia wanapochimba udongo na changalawe wazingatie taratibu na kutochimba kando ya barabara, na kuwasihi pale malipo yao yanapochelewa wawe wavumilivu wakati serikali ikiendelea kuwashughulikia, na kwamba katika uandishi wa mabango ya kutambulisha miradi waandike kwa lugha ya kiswahili.

Awali Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Avith Theodory, akisoma taarifa amesema,wakandarasi walioshinda zabuni za matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja ni 21,na mikataba ambayo ina sainiwa ni 33, yenye thamani ya sh.bilioni 10.2.

Amesema mikataba hiyo ni ya utekelezaji wa miezi 12, na kwamba fedha zake ni vyanzo vya mfuko wa barabara, tozo za mafuta pamoja na mfuko wa jimbo,na barabara ambazo zitafanyiwa matengenezo ni urefu wa kilomita 716.64, ujenzi wa makalvati 381,madaraja 4,mitaro urefu wa mita 5,280, pamoja ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilomita 2.8 na uwekaji wa taa za barabarani.

Mmoja wa wakandarasi kutoka kampuni ya Gapro Construction Limited Mhandisi Amedeus Mselle,ameishukuru Serikali kwa kuwa amini wakandarasi wazawa, na kwamba watafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa na kukamilisha kwa wakati.