MTIA saini namba 55 katika waraka wa watia nia wa ubunge 55 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) 2025, maarufu kama G55 James Kabepele, amekana kuhusika katika waraka huo akiwataja wahusika kuwa ni wasaliti wa Chama.
Kabepele ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora amekanusha kuhusika na waraka huo wa vuguvugu la G55 linalodaiwa kupinga kampeni ya 'No Reforms No Election', na kusema kuwa hakuwahi kuweka saini kwenye waraka huo wala kuonesha nia ya kugombea jimbo lolote.
Kabepele amesema kuwa waraka huo unaotaja jina lake kama mtia nia wa Jimbo la Igalula, pamoja na saini inayodaiwa kuwa yake, si wa kweli na haukuwahi kupata ridhaa yake.
“Mimi si mtia nia wa jimbo lolote, na sikuwahi kuweka saini kwenye waraka huo. Siwezi kujua nani aliweka saini hiyo kwani ni rahisi kughushi kwa sababu ya nafasi yangu na ushiriki wangu katika vikao mbalimbali vikubwa,” amesema Kabepele
Amesema kuwa haipingi kampeni ya No Reforms No Election na kuwa hakuna mgawanyiko katika uongozi wa CHADEMA mkoa wa Tabora.
Amesema Tabora wanashirikiana kwa pamoja kutekeleza ajenda ya chama na kusukuma mbele kampeni hiyo ya mageuzi kabla ya uchaguzi.
“Hii siyo ishu ya mtu mmoja mmoja. Mkoa wa Tabora tumeungana, tunasubiri miongozo ya kitaifua, na tunatekeleza yale tuliyokubaliana kama chama,” amesema.
Aidha Kabepele amesema wanaendelea na maandalizi ya mapokezi ya ziara ya viongozi wakuu wa CHADEMA akiwamo Tundu Lissu na John Heche ambayo kwa umoja yamepangwa kupitia kamati maalum za maandalizi, kufuatia maazimio ya Baraza la Mashauriano.
Ameeleza kuwa viongozi hao wanatarajiwa kuwasili Tabora kama sehemu ya ziara ya Kanda ya Magharibi kwa ajili ya kuhamasisha ajenda ya No Reforms No Election na kampeni ya Tone Tone, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi.
Amedai si yeye pekee aliyeghushiwa saini kwenye waraka huo, bali kuna viongozi wengine wa mkoa wa Tabora waliokumbwa na hali kama hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED