TAARIFA ‘mbaya’ kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ni kwamba ulaji wa nyama nyekundu, vyakula vya kusindika, vyenye mafuta mengi bila matunda na mboga, umeongeza wagonjwa wa saratani ya utumbo mpana.
Saratani hii imeongezeka nchini, ikitajwa kuwaathiri vijana kuanzia miaka 40. Hata hivyo, saratani ya kizazi na matiti, bado inaongoza.
Akizungumza na Nipashe Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage, alisema kwa wastani hospitali hiyo inapokea wagonjwa watatu wa saratani ya utumbo mpana kila siku.
Dk. Mwaiselage anasema miaka 10 iliyopita, aina hiyo ya saratani haikuwa inatajwa nchini, lakini hivi sasa ipo kwenye orodha ya aina 10 tishio. Anasema kuna ongezeko la aina hiyo ya saratani duniani.
“Tanzania imeongezeka sana na inatokea katika umri mdogo. Zamani ilikuwa inatokea katika umri mkubwa, lakini miaka ya karibuni inatokea kwa watu wenye umri mdogo.
“Chanzo cha kwanza ni kama kuna historia kwenye familia, cha pili ni mtindo wa maisha hasa ulaji usiofaa kama matumizi ya nyama nyekundu, vyakula vilivyosindikwa, vyenye mafuta (unene), kutokula matunda na mboga mboga.
“Tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ilikuwa inatokea kwa watu wenye miaka 60 na kuendelea, Tanzania inatokea wastani wa miaka 40. Umri wa katikati wa kufanya kazi,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk. Mwaiselage, takwimu zinaonesha kwamba wastani wa umri wa watu kupata saratani nchini ni miaka 45 hadi 50, wengi wakiwa wanawake wanaopata kwenye mlango wa kizazi na matiti.
Anasema mbali ya ongezeko la wagonjwa wa saratani ya utumbo mpana, saratani zinazoongoza nchini na asilimia kwenye mabano ni ya shingo ya kizazi (35), matiti (15), njia ya chakula (10), ngozi (TISA), muunganiko wa saratani ya kichwani, mdomoni na shingoni (nane), tezi dume (saba) na utumbo mpana (sita).
Hali hiyo, anasema inatokea pia kwenye nchi zilizoendelea kama Marekani na Ulaya, ambako raia wa nchi hizo walikuwa wanapata saratani wakiwa na umri mkubwa kuanzia miaka 60 hadi 90 na kwamba kwa sasa wagonjwa wanabainika hata katika umri wa miaka 50.
Anasema kwa nchi kama Marekani wanapata saratani katika umri mdogo kwa sababu ya kuongezeka kwa visababishi vya saratani na jitihada za kugundua ugonjwa huo mapema.
Taarifa hiyo ya Dk. Mwaiselage inakuja siku chache baada ya Jumuiya ya Saratani ya Marekani, kubaini kwamba vijana wa kike wako hatarini kupata saratani.
"Saratani ya matiti huchangia karibu nusu ya uchunguzi wote wa saratani kwa wanawake walio na umri wa chini ya miaka 50," alisema Rebecca Siegel, mwandishi mkuu wa utafiti huo na mkurugenzi mkuu wa kisayansi wa utafiti wa jumuiya hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED