KILA zama na kitabu chake. Mambo yanakwenda yakibadilika. Miaka ya 1970, hadi mwanzoni mwa miaka 2000, usafiri wa haraka ulikuwa ni wa taxi. Mtu akitaka kwenda mahala ambako anadhani usafiri wa umma, Uda au daladala atachelewa, atakachofanya ni kwenda kwenye kituo cha taxi.
Usafiri huo utakupeleka popote pale unapokwenda kwa haraka na usalama zaidi kwani utakufikisha pale pale ulipotarajia kufika. Kama ni nyumbani, ofisini, kumbi za starehe, baa, hoteli, hospitali au kwenye ahadi yoyote. Halafu enzi hizo mtu ambaye anakodisha taxi, alionekana ni mwenye uwezo wa kifedha.
Kulikuwa na maeneo maalum ambapo magari hayo yalikuwa yakipaki kusubiri wateja. Vilijulikana kama vitu vya taxi. Vilikuwa maarufu sana kama stendi ya basi zilivyokuwa. Aina ya magari yaliyotumiwa kwa wakati huo, ni Peugeot 404, na baadaye zikaja 504, ambazo watoto wa mjini walikuwa wakiziita 'guruwe'.
Kwa kipindi cha miongo mitatu, kuanzia 1970, 1980, 1990, aina hiyo ya magari ndiyo yaliyotumika sana kwa taxi, lakini baada ya hapo wakati taxi zinaanza karatibu kupungua, kulikuwa na aina tofauti tofauti, lakini Toyota Corolla, ndiyo zilikuwa nyingi zaidi.
Madereva wa taxi kwa wakati huo walikuwa wanajulikana hata kwa majina. Walikuwa ni watu maarufu kwa maeneo wanayoweka vituo vyao.
Wengi walijulikana kutokana na kazi zao hizo za kusafirisha watu kwa njia hiyo.
Ingawa biashara hiyo bado ipo, lakini imedorora kwa kiasi kikubwa, haipo kama zamani. Kwa sasa dereva taxi ni kazi ambayo kama hutokuwa makini, au hauna watu wako basi utakufa njaa. Biashara hiyo kwa sasa ipo kwenye sehemu muhimu sana kama kwenye mahoteli makubwa, viwanja vya ndege na sehemu zingine zinazofanana na hiyo.
Ukiondoa hapo, sehemu zingine biashara ya taxi imeanza kufa kifo cha asili.
Uwepo na bajaj na bodaboda umeonekana kuondoa kwa kasi biashara ya taxi kwenye ulingo wa biashara.
Zilianza kama utani tu, mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini kwa sasa zimeshamiri kila kona na pembe ya nchi na kuwa usafiri wa kawaida kabisa kwa watu wote. Tofauti na zamani ambapo anayekodisha taxi anaonekana kibopa, lakini usafiri wa bodaboda na bajaj kwa sasa umekuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida kwa watu wote, hao wenye hali ya chini ndiyo kabisa wana uhitaji zaidi.
Kupanuka kwa miji, hasa sehemu ambazo hazina usafiri ya mabasi au miundombinu ya barabara, kumesababisha bodaboda kuchukua nafasi yake.
Mfano jijini Dar es Salaam, mji ulikuwa unaishia Ubungo, lakini kwa sasa maeneo ambayo zamani walikuwa mashamba kama Sinza, Kunduchi, Goba, Boko, Bunju, Gongolamboto kuwa majumba, na ukiteremka kwenye barabara kubwa unaingia ndani tena ambako kunakuwa na usafiri na bajaj na bodaboda tu.
Foleni za magari kwenye miji mikuu pia zimesababisha bajaj, na bodaboda kujichukuliwa 'ujiko', kwani unakuwa ndiyo usafiri wa haraka, kutokana na kutokaa foleni na kuweza kupita sehemu mbalimbali finyu, ambazo mabasi na magari madogo hayawezi.
Tuma meseji 0716 350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED