LATRA yakamata magari 20 kutoza nauli kubwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:58 AM Jan 04 2025
Stendi ya Tabora.
Picha:Mtandao
Stendi ya Tabora.

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Tabora, imeyakamata magari 20 yanayofanya safari kutoka Tabora mjini kwenda wilayani Sikonge kwa kutoza abiria nauli kubwa kupita kiwango kinachotakiwa kisheria kwa madai ya gharama za uendeshaji kuongezeka.

  , akitoa taarifa kwa gazeti hili alisema kuwa magari hayo wameyakamata kutokana na ukaguzi walioufanya na kubaini yanatoza nauli kati ya Sh. 4,000 hadi Sh. 5,000 badala ya Sh. 3,700 inayotambulika kisheria.

Mmari alisema kuwa katika ukaguzi huo wamegundua wahusika wa magari hayo wamekuwa hawarudishi chenji kwa abiria wanapotoa pesa ili kulipa nauli na kwamba wamekuwa hawawapi tiketi zinazoonesha malipo halisi.

“Serikali ilitangaza nauli halali Desemba mwaka 2023 na kuanza kutumika nchi nzima na mkoani Tabora tulimwambia Mkuu wa Mkoa ambaye aliwaita wadau wote wa usafirishaji na kuwaeleza na kuwahimiza kufuata sheria zote za umiliki wa vyombo vyao,” alisema.

Alisema kuna magari kati ya 50 hadi 70 yanayotoa huduma ya usafirishaji toka Tabora mjini kwenda wilayani Sikonge na kuna umbali wa kilomita 77 na kama wamiliki wa magari watafuata sheria zilizopo na kuwafuatilia watu waliowaweka kusimamia magari yao watapata faida kubwa zaidi.

Ofisa mfawidhi huyo alisema kuwa magari yote yanayofanya shughuli za usafirishaji yanatakiwa kuwa na mkanda wenye rangi yake kulingana na uelekeo waliopangiwa kwa magari yanaenda wilayani Sikonge yanatakiwa kuwa na mkanda wa rangi ya kijani na ubavuni kuandikwe nauli inayotakiwa pamoja na eneo linapotoka na kuelekea.

“Magari yote yanatakiwa kuwa na tiketi, yale makubwa watoe tiketi za kielektroniki na haya ya wilayani yanatakiwa kutoa tiketi zinazoonesha namba za gari, jina la kampuni, jina la abiria, siti yake na kiwango cha nauli na hii inasaidia kuonesha nauli halali inayotozwa, kulitambulisha gari na kumtambulisha abiria alipotoka na anapokwenda,” alisema.

Alisisitiza kuwa wamiliki na madereva wa magari wasisingizie kupanda au kushuka kwa gharama za mafuta ili kupandisha nauli na kwamba gharama za uendeshaji sio mafuta pekee ni pamoja na vipuli na malipo ya wafanyakazi na mambo mengine ambayo ni ya kawaida,” alisema.

Mmari aliwataka kufuata sheria za usafirishaji kwa kuvaa sare za kaunda suti za rangi ya bluu ama tisheti zenye nembo ya kampuni, kutoza nauli halali na kutoa tiketi za kieletroniki na wanatoa tiketi za kawaida wahakikishe zinakuwa vigezo vyote na watambue serikali ndio yenye mamlaka ya kutangaza mabadiliko ya nauli.

Aidha, aliwataka wamiliki wa magari kutotumia wapigadebe ama vishoka kuwakatia tiketia abiria kwa kuwa wanawaumiza na ni kinyume cha sheria na kwamba wanawaongezea gharama za uendeshaji kwa kupigwa faini watakapobainika na kukamatwa na watu hao wanajinufaisha kupitia mali zao.

Alisema mabasi yapo ya kutosha, hakuna tatizo la upungufu na kwamba abiria wahakikishe wanalipa nauli zao wanapoona basi husika lipo kituoni na wapande na kuingia ndani ili wahudumiwe kwa kulipa nauli zao halali nakupatiwa tiketi halisi.