WAKATI minyukano ikiendelea kati ya ngome ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Makamu wake, Tundu Lissu, mgombea wa tatu wa nafasi ya uenyekiti wa chama taifa, Charles Odero amesema kinachoendelea ni ukiukwaji wa Katiba ya chama hicho.
Miongoni mwa vitu alivyodai Odero kuwa ni ukiukwaji matakwa ya kikatiba ni wagombea hao kuwa na wenza katika uchaguzi huo, makundi, kuunda timu, kuanza kampeni kabla ya muda pamoja na kutangaza kura kinyume cha utaratibu.
Odero ambaye tayari amechukua fomu kuwania kiti hicho, alibainisha hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na Nipashe iliyotaka kujua kilicho nyuma ya ukimya wake baada ya kuchukua fomu licha ya wenzake kuonekana mara kwa mara hadharani.
Alisema Katiba ya chama hicho imeweka wazi nafasi zinazotakiwa kuwaniwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ambao wamegawanyika katika makundi matatu.
"Makundi hayo ni ya wanawake, wenye ulemavu pamoja na kundi mchanganyiko lakini hawa wenzangu wamekwenda mbali zaidi wamekuwa na kundi la mgombea na mgombea mwenza ambalo katiba ya chama haitambui hilo," alidai.
Odero alitaja jambo lingine analoona wagombea wenzake wanakiuka Katiba ya chama chao ni kutengeneza mtandao, akitolea mfano mtandao unaomuunga mkono Lissu pamoja na mtandao wa Mbowe.
"Si kwamba Katiba haijatoa mwanga kuhusu makundi, lakini katika uchaguzi huu imebainisha kuwa kila mgombea anatakiwa kugombea kama yeye na wala si kutengeneza makundi wala mtandao wa kuweza kupata uongozi," alisema Odero.
Aidha alitaja ukiukwaji mwingine wa Katiba ya chama chao ni baadhi ya wajumbe kutangaza wazi kura zao kupitia vyombo vya habari ilhali kura katika uchaguzi huo ni siri.
"Tumeona kwenye mikoa watu wanajitokeza wanasema 'sisi kura yetu ni kwa fulani', suala hili si sahihi kikatiba na kwa mujibu wa taratibu za kichama hazijaruhusu kampeni, lakini kinachoendelea kinaonesha ni kwa namna gani wananadiana," alisema Odero.
Alisema kuwa katika uchaguzi huo kila mmoja ana nafasi yake na akiipata atatakiwa kuitumikia kama yeye na wala si kwa msaada wa msaidizi wake kwa kuwa Katiba imebainisha kila nafasi na majukumu ya mhusika na wote watakutana katika Kamati Kuu.
Kuhusu Lissu kudaiwa kukichafua chama hicho kipitia tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya viongozi, Odero alisema Katiba haijamzuia mtu yeyote kutoka nje na kueleza maoni yake.
Hata hivyo, Odero alisema licha ya Lissu kuwa mwanasheria na kiongozi katika chama hicho, anatakiwa kufuata njia sahihi za kiuongozi kuwasilisha jambo hilo ikiwa ni pamoja na kulifikisha kwenye uongozi pamoja na taasisi za serikali ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kama kuna wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na si kuishia kuongea kwenye majukwaa.
Alisema kuwa katika mambo yanayohusiana na rushwa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, mhusika anaweza kupewa onyo, kuvuliwa uongozi na hata kufukuzwa uanachama.
Kuhusu sababu ya yeye kugombea nafasi hiyo, Odero alijitambulisha kuwa "ni sura mpya ndani ya chama", anahitaji kuwaleta wana- CHADEMA pamoja na kuwa wamoja kueleka katika Uchaguzi Mkuu na ujenzi wa chama hicho.
"Nitawaweka pamoja wanachama wote, umma wa watanzania pamoja na viongozi wa chama chetu kuelekea katika mchezo pekee ambao kwetu mpinzani mkubwa ni CCM (Chama Cha Mapinduzi)," alisema Odero.
Alisema viongozi hao wanaochuana wameongoza kwa muda mrefu, hivyo ni wakati wa kuachia nafasi kwa sura mpya na fikra mpya ili kupeleka chama hicho mbali zaidi.
"Lissu na Mbowe wamekuwa kwenye uongozi wa chama hiki kwa zaidi ya miaka 24 sasa, sidhani kama wana fikra na maono mapya ambayo yatakayokifanya chama kuwa kipya, hivyo chama kinamhitaji Odero kwa ajili ya mageuzi," alisema Odero.
Kwa mujibu wa kanuni za kuendesha kampeni za ndani ya chama hicho, kanuni ya 2.0 (i-vii), ni kosa kwa mgombea au wakala kufanya kampeni kabla ya muda, kufanya kampeni chafu kwa kukashfu wagombea wengine kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, kuhusisha ukanda, udini, ukabila au ubaguzi wa aina yoyote ile.
Vilevile, kanuni hizo pia zinaelekeza kuzingatiwa kwa masharti yaliyoainishwa katika mwongozo dhidi ya rushwa pamoja na kutokufanya kampeni kwa kujinasibu na kiongozi yeyote wa kitaifa, wilaya au kiongozi yeyote wa kuchaguliwa iwe kwa mazuri au mabaya.
Kifungu cha 3.0(i-v) kinaainisha adhabu dhidi ya ukiukwaji kanuni hizo kuwa ni pamoja na mhusika kupewa onyo, kupewa onyo kali au kuondolewa katika mchakato wa uchaguzi iwapo itathibitika kuwa mgombea amekiuka utaratibu wa kampeni kwa mujibu wa mwongozo huo.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa CHADEMA hicho, John Mnyika aliwaonya wanachama, wagombea na mawakala wao dhidi ya ukiukwaji sheria na miongozo ya chama, akidokeza kuwa moja ya adhabu ni kuondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED