Rais Samia atunukiwa tuzo akiahidi utumishi mwema

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:20 PM Apr 06 2025
Rais Samia Suluhu Hassan
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametunikiwa Tuzo ya Mwanamke Kinara 2025, iliyotolewa na wanawake wa Kanda ya Ziwa, kwa kutambua mchango wake kwenye sekta mbalimbali.

Tuzo hiyo imepokelewa usiku wa Aprili 5, 2025, jijini Mwanza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, wakati hafla hiyo ikiendelea Rais Samia alipiga simu kuwashukuru.

"Nawashukuru sana kwa tuzo hii,mmenipa ushirikiano nikaweza kuyafanya yanayotakiwa kwenye elimu, afya, maji na umeme," amesema.

"Nawashukuru sana akinamama kwa utulivu wenu na kunipa moyo. Ahadi yangu kwenu sitawaangusha, nitawatumikia kadri Mungu atakavyoniwezesha," amesema Rais Samia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alipokea tuzo hiyo kwa niaba
Tuzo hizo zimeandaliwa na wanawake 500, ambao ni wajasiriamali na wafanyabiashara kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Geita na Simiyu) pamoja na mikoa miwili ya Kanda ya Magharibi (Kigoma na Tabora), hivyo jumla ni mikoa minane.

Aidha, wanawake wengine 16 walitambuliwa kwa kuwa vinara katika maeneo mbalimbali ya kazi kwa Kanda ya Ziwa.

Tuzo hizo ambazo zimeingia msimu wake wa tano mwaka huu, zimepewa jina la Rais Samia, kwa lengo la kutambua mchango wake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania, hususan wanawake wa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.

Awali, Mwanzilishi na Mwandaaji wa Tuzo za Samia Mwanamke Kinara, Khadija Liganga, amesema Rais Samia umekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea shughuli za uzalishaji, ujasiriamali na maendeleo ya kijamii kwa wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alipokea tuzo hiyo kwa niaba
Amesema miradi hiyo imekuwa mkombozi kwa wanawake wengi waliokuwa pembezoni mwa mfumo rasmi wa uchumi.

“Tumeona ni jambo la heshima na faraja kubwa kuenzi uongozi wa Rais wetu, kwa kumpatia tuzo hii maalum. Kupitia dira yake ya maendeleo jumuishi, wanawake wamewezeshwa, wamehamasika na sasa ni kinara wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi,” amesema Khadija.

Katika hafla hiyo, jumla ya wanawake 16 kutoka mikoa minane; Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Kagera, Mara, Tabora na Kigoma walitunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na mchango wao katika sekta za uongozi, biashara, kilimo, elimu, afya na ustawi wa jamii.

Aidha katika hafla hiyo, baadhi ya waandishi wa habari wanawake walitunukiwa tuzo.