WATU sita wakiwamo walimu wanne wa Shule ya Msingi Lumalu, kata ya Upolo, Nyasa mkoani Ruvuma, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka katika cha kijiji Upolo kwenda Kilosa Mbambabay, kuungua moto.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana saa 2:00 asubuhi katika eneo la kona za Chunya inapopita barabara inayotoka Mbinga - Mbambabay.
Alisema watu hao walipata ajali wakiwa njiani kwenda kwenye usaili wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura. Gari hilo aina ya Toyota Prado liliacha njia na kugonga gema la barabara kisha kupinduka na kuwaka moto.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kilichosababisha watu hao kushindwa kujiokoa na kuungua moto ni milango ya gari hilo kujifunga.
“Jitihada mbalimbali zilifanyika, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilikwenda kwenye eneo la tukio kuona namna ya kuondoa miili ya marehemu hao na kuisafirisha kwenda hospitali ya serikali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya taratibu za kufanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili miili ikabidhiwe kwa ndugu zao,” alisema.
Magiri aliwataja waliofariki dunia kuwa ni dereva na mmiliki wa gari hilo, Vincent Milinga, na walimu Damas Nambombe, Dominika Ndau, Judith Nyoni, Sylvester Mtuhi na mfamasia Boniface Mapunda.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu zaidi ya mara mbili bila kupokewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED