WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, ameeleza namna anavyofurahishwa na Umoja wa Wakazi wa Rombo (RU) wanaoishi ndani na nje ya Tanzania, wanavyopambana kusaidiana katika misiba na kunyanyuana kwa kupeana mitaji, huku akichombeza kuanzishwa harambee kuchangia watoto wanaohitaji kusoma.
Akizungumza jana Disemba 27, 2024 katika mkutano wa kwanza wa Rombo Unity uliofanyika eneo la Mashati, Kata ya Katangara Mrere, Wilayani humo, ameshauri kama mtu ana mtoto wake amefaulu vizuri, asaidiwe kusoma.
Prof. Mkenda amesema, “Kuendesha taasisi kama hii (Rombo Unity), sio jambo rahisi, misukosuko mliyopitia naifahamu, kwa sababu mimi nilikuwa nafuatilia.
“Kenya tangu zamani walikuwa na harambee za kusomesha watoto. Harambee imeendeshwa na Mbunge, kumsaidia mtoto fulani kwenda kusoma Marekani. Harambee imeendeshwa kusaidia fulani kwenda kutibiwa, tumeona kwa wenzetu wamesoma na wameenda kwa kasi zaidi.
Zaidi aliongeza: “Hasa kikundi kama hiki na vingine tunachohitaji kama wanavyosema wataalam, sisemi kwamba mimi ni mtaalamu. Tutafute namna na mkakati ambao tunaweza tukafika mbali zaidi.
Mojawapo mtu kabla hajafa, namna gani atatibiwa. Sio rahisi kwa sababu udanganyifu bado upo lakini ni jambo ambalo lazima tuliangalie. Ni bima ya afya tunaendaje, la kwanza kuzuia kifo, la pili kuzikana.”
Na mimi nikitoka hapa naweka zangu milioni moja ili kuhakikisha kwamba tunasonga mbele.Nitausemea, kuhamasiha na tusikate tamaa.
Mwenyekiti wa Rombo Unity, Cleophas Mrina, akizungumza katika mkutano huo amesema umoja huo uliofikisha wanachama hai 410, katika kipindi cha miezi 20 toka kuanzishwa, imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh. milioni 240.33.
Mrina, ameeleza kuwa moja ya mikakati yao ni kuanzisha pia baraza la ushauri, ambalo litasimamia masuala yote ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED