WATAALAM na wadau wa mazingira nchini wameishauri wizara kuja na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari za ukame ikiwamo teknolojia za kisasa za kuvuna na kuhifadhi maji, chakula na kuhamasisha uhifadhi wa uoto wa asili.
Hayo yamesemwa ikiwa ni wiki mbili tangu ripoti iliyotolewa na Mpango wa Kudhibiti Kuenea kwa Jangwa na Ukame duniani (UNCCD), iliyoitwa Tishio la Kimataifa la Kukauka kwa ardhi; Mwelekeo wa Ukame wa Kikanda na Ulimwenguni na Makadirio ya Baadaye, kuzitaja nchi za Tanzania na Sudan Kusini, kuwa zinaelekea kwenye ukame kwa kasi kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine ulimwenguni.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Desemba 9, mwaka huu katika mkutano wa 16 nchi wanachama wa UNDCC (COP 16) uliofanyika Riyadh, Saud Arabia, Novemba 30 hadi De semba 14, mwaka huu, (COP16) ilionyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la ukame ulimwenguni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo kama hali ya ukame ikiendelea kuongezeka itasababisha madhara makuwa ikiwamo uharibifu wa mifumo ya ikolojia ikiwamo ardhi kukosa rutuba na kusababisha kudorora kwa kilimo.
Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Pius Yanda, alisema ni vigumu kuzuia ukame usitokee nchini kwa sababu unachochewa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaikabili dunia kwa sasa.
Alisema ili kupunguza makali ya athari za ukame na jangwa kama nchi, wizara zinapaswa zijipange na kufanya kazi kwa kushirikiana na kuja na mikakati ya kuleta uhimilivu.
Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni kuhakikisha kuwa kipindi ambacho mvua zipo za kutosha uzalishaji wa chakula uwe wa juu ili kihifadhiwe cha kutosha kitumike kipindi ambacho uzalishaji ni mdogo kutokana na mvua kuwa chache.
Alisema pia serikali na wadau wahamasishe teknolojia ya kisasa ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kulisha mifugo ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea kutokana na ukame kama migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Pia, inapaswa kujiandaa na kuja na mbinu bora za kutatua migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na ukame ikiwamo ya wafugaji na wakulima akisisitiza njia hizo zinapaswa kuwa za kuyanufaisha makundi yote kwa usawa.
Aliishauri pia serikali ijipange kudhibiti vijana kukimbilia mijini na kusasababisha msongamano mkubwa wa watu na kuongeza athari za ukame kama vile maji kuadimika.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mikakati ya Maendeleo Endelevu (TSDI), Fredy Kwezi, alisema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa mazingira kupanda miti ili kudhibiti athari za mabadiliko ta tabianchi yanayochochea ukame, matokeo bado hayaridhishi.
Alitaja sababu za kutoridhishwa kwa matokeo hayo kuwa wadau hao wamejikita zaidi kwenye kupanda miti, lakini hawarudi kuangalia kama miti hiyo imestawi au la na namna ya kuitunza.
Fredy aliyehudhuria COP16 akiiwakilisha nchi, alisema hali hiyo inasababisha miradi mingi ya upandaji miti kufeli kwa sababu wadau wa shughuli hiyo wakishapanda mti wanapiga picha na kurusha mitandaoni na kuishia hapo.
Alisema njia sahihi ya kupanda miti ikastawi na kuleta matokeo chanja ni kushirikisha wataalam ili kufahamu ni aina gani ya miti ipandwe katika eneo fulani.
"Kwa sababu miti inayostawi vizuri Njombe huwezi kuipanda Dar es Salaam, na inayostawi vizuri Pwani huwezi kwenda kuipanda Mbeya," alisema.
Alitaja pia njia ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kama suluhisho la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa ikitumika vizuri inasaidia kuzuia vivutio vya ukame kama vile mmomonyoko wa udongo.
Mtaalam wa mabadiliko ya tabianchi Nyendo Kinyonga, alisema kuna haja ya kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa kuhusu ukame na visababishi vyake na namna ya kukabiliana nao, ili jamii ichukue nafasi yake kujikinga badala ya kutegegemea mamlaka.
Alisema suala hili liachiwa mamlaka za kiserikali pekee kama vile Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Wakala wa Misitu matokeo hayatakuwa tarajiwa na ukame utazidi kuongezeka na kwamba kila mmoja anapaswa awajibike kwa nafasi yake.
"Kwa mfano kwa sasa hivi kuna changamoto ya wakulima kusafisha mashamba kwa kuyachoma moto, hii izalisha sana hewa ya kaboni inayochochea athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwamo joto kali na kusababisha ukame," alifafanua.
Alishauri pia wakulima wajikite kwenye kilimo cha zamani ambacho kilikuwa hakitumii mbolea kutokana na matumizi ya viuatilifu kuharibu udongo, na kuchochea ukame.
Mkugenzi wa Taasisi ya Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), Sarah Pima, alisema jitihada za pamoja zinahitajika katika nchi za Jangwa la Sahara ili kukabiliana na ukame.
Alisema kwa upande wa Tanzania kunahitajika sera madhubuti za kukabiliana na jangwa ikiwamo kuongeza kiwango cha kuhifadhi uoto wa asili na misitu iliyopo badala ya kuegemea kwenye kupanda miti pekee.
Aliwasihi wananchi kulichukuliwa suala la jangwa na ukame kwa uzito kwa sababu athari zinazidi kuongezeka, mikakati ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi itekelezwa sasa badala ya kusubiri hali ikiwa mbaya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukame ni chanzo kikuu cha uharibifu wa ardhi, ukiharibu takriban asilimia 40 ya ardhi yenye rutuba duniani, hivyo kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa kilimo na uhaba wa chakula.
Ilieleza pia barani Afrika, kuongezeka kwa ukame kumehusishwa na kupungua pato la taifa kwa asilimia 12 kati ya mwaka 1990 na 2015, jambo linaloonyesha changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na uharibifu wa ardhi.
Kupitia michango iliyoamuliwa Kitaifa (Nationally Determined Contribution - NDC), Tanzania imeahidi kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa kiwango cha asilimia 30 hadi 35 katika sekta zote za uchumi, ikilinganishwa na hali ya Kawaida ifikapo mwaka 2030.
Hali hiyo inatarajiwa kupunguza takriban tani milioni 138-153 za kaboni dayoksaidi (MtCO2e) kwa jumla, kutegemeana na maboresho ya ufanisi wa msingi, sambamba na ajenda yake ya maendeleo endelevu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED