JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefafanua tukio la bajaji kuwaka moto, baada ya kukamatwa na polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Aprili 4, 2025 majira ya asubuhi, eneo la Ubungo-Mawasiliano, askari Polisi wakiwa katika utekelezaji wao wa sheria za usalama barabarani katika eneo Kimara Baruti, walimkamata dereva bajaji aitwaye John Mosha (30), mkazi wa Kimara Temboni.
Dereva huyo alikamatwa kwa kosa la kupita katika barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT) akiwa na bajaji yenye namba za usajili MC 427 DTZ.
"Dereva huyo wa bajaji wakati wa ukamataji awali alikaidi amri ya kukamatwa na kuamua kuendesha bajaji kwa mwendokasi bila kusimama hadi maeneo ya Ubungo-Mawasiliano, alipokamatwa.
"Baadaye madereva wenzake wa bajaji walifika na kuanza kuwazuia askari Polisi kumshikilia dereva huyo. Mmoja kati ya madereva hao alichomoa Plag ya Pikipiki ili isichukuliwe na Polisi kitendo kilicho sababisha cheche na hatimaye moto kuwaka kwenye bajaji hiyo."
"Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, linatoa onyo kali kwa madereva wole wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani na kuacha mara moja kupita kwenye barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT), isipokuwa yale magari yaliyoruhusiwa kisheria," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED