MACHI kila mwaka ni ‘mwezi wa kinamama’ na Siku ya Wanawake Duniani inafikia kilele Jumamosi Machi 8.
Kwa Tanzania mwaka huu maadhimisho yanafanyika Arusha, jicho la kinamama na wadau wengine linaangazia Ulingo wa Beijing na maazimio yake baada ya miaka 30 ya kufanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake waliokutana China, 1995.
Wakati wa kutafakari miaka 30 au Beijing +30 ikumbukwe Mratibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing ni Balozi Getrude Mongela, ambaye ameandika historia kutetea haki za mtoto wa kike, msichana na wanawake duniani kote.
Ndiyo maana wakati umefika wa kuitangaza rasmi kitaifa siku ya kumuenzi kwa mchango mkubwa utakaodumu miongo mingi wa kutetea na kulinda haki za wanawake, mtoto wa kike na za binadamu, ni mapendekezo ya baadhi ya wanaharakati.
Akizungumzia azma ya kumuenzi Mama Mongela, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya KIOTA, Justa Mwaituka, anasema wakati umefika kumpa siku maalumu ya kufurahia na kuuenzi kazi zilizotukuka alizofanya kwenye Mkutano wa Beijing.
“Mwanamama huyo hawezi kusahaulika kwa kutetea utu, ulinzi, heshima na pia kuhimiza harakati za mataifa duniani kushikamana kuwainua wanawake na watoto wa kike kuanzia Tanzania, Afrika na duniani kote.”
“Amefanya makubwa. Ameandika historia itakumbukwa ameongoza sekretarieti ya mkutano huo kwa mafanikio. Amesimama kuiitetea, kuisimamia na kuiingiza ajenda ya kumwezesha mtoto wa kike kwenye maazimio 12 ya mkutano wa Beijing mwaka 1995. Hili haliwezi kusahaulika” anakumbusha Justa.
Justa, muuguzi kitaaluma alianzisha taasisi ya KIOTA mwaka 1998, miaka mitatu baada ya mkutano wa Beijing, ukiwa ni mwendelezo wa kazi za Mama Mongela, kusaidia watoto wa kike, wasichana na wanawake wenye umri mkubwa ili kuwaondoa kwenye unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kuwawezesha kiuchumi.
Anasema Mama Mongela alifanya kazi kazi na kuonyesha dunia kuwa wanawake wanaweza na mambo aliyoyafanya yalipokelewa na Umoja wa Mataifa na kufanyiwa kazi na mataifa wanachama wa UN.
Aidha, kazi yake imechangia au kuchochea usawa wa kijinsia kwenye masuala yote ukizingatiwa wenye juhudi za kutafuta maendeleo ya kila jamii.
Ni wazi kuwa kwa miaka 30 iliyopita sauti za wanawake na watoto wa kike na changamoto zao zimejulikana bayana na kutafutiwa ufumbuzi kwa kuingiza usawa wa kijinsia kwenye karibu sekta zote.
Anakumbusha kuwa kwa Umoja wa Mataifa usawa wa kijinsia umekuwa suala mtambuka mfano malengo ya milenia na sasa malengo ya maendeleo endelevu usawa huo ni lazima kuzingatiwa kwenye hatua zote za maendeleo huku hali ya wanawake na watoto wa kike ikitazamwa kwa jicho maalumu.
Mshiriki wa mkutano wa Beijing Mary Rusimbi, anasema mwaka huu maadhimisho yanapofanyika Watanzania wanapaswa pia kusherehekea mchakato wa kimapinduzi uliofanywa na Mama Mongela, aliyeongoza sekretariati.
Anazichangia kazi za Mongela kwa kuingiza ajenda ya Afrika ya kumwezesha mtoto wa kike kwenye maazimio 12 ya mkutano huo na ikiwa moja ya ajenda kuu na kisha azimio la kidunia la kumwangalia mtoto huyo aliyewekwa nyuma kwenye kila eneo kuanzia elimu, lishe na afya .
Aidha, alikuwa mwathirika wa mila potofu na desturi mfano, unyanyasaji kingono, ndoa za utotoni, ukeketaji. Pia, sera na sheria kandamizi yote hayo yakimrudisha nyuma mtoto wa kike hasa wa Afrika.
Anasema lakini kwa ujasiri Mongela, alilizungumzia suala hilo akihamasisha upatikanaji wa fedha ili kumwezesha mtoto wa kike na kumuondoa kwenye unyanyasaji.
Marry ambaye ni miongoni mwa wanaharakati waliozunguka mikoani kukusanya maoni ili kuandaa ajenda za Tanzania na pia mshiriki wa mkutano huo,anasema Mongela aliongeza ufahamu, uelewa kwa dunia kujua hali ilivyokuwa kwa mtoto huyo, mambo ambayo yalikuwa hayafahamiki.
Anasema kupitia juhudi hizo amesaidia dunia kujua kuwa sehemu nyingi watoto walifanyiwa ukatili unyanyasaji, hawakuwa na haki ya kusoma , kurithi, kufanya kazi, kuamua hatima ya maisha yao na sasa wamepata ukombozi na sauti zao zinasikika, licha ya kwamba mapambano yanaendelea kufikia haki sawa kwa mtoto wa kike na wanawake.
Anaongeza kuwa maono yake yalikuwa kusimamia maendeleo ya wanawake na mtoto huyo kwa sababu ndizo nguzo za kuendeleza taifa.
Anastahili kulindwa kisheria, kisera na kimiongozo ili aelimishwe, atibiwe, awezeshwe kiuchumi, ashiriki kwenye matumizi ya rasilimali na maamuzi ya maendeleo kwenye jamii kwa sababu ni mhimili mkuu wa jamii yoyote.
Mama Mongela aliona kuwa bila kumjali mama na mtoto wa kike , kumpa heshima, hadhi na mitizamo mipya katika jamii, huenda dunia ingeyumba.
Anasema baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na Mkutano wa Beijing ambao Mongela aliuratibu, yameleta mabadiliko na kuendelea kuenzi mtoto wa kike , mfano Siku ya Mtoto wa Kike Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Oktoba 11. Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2012 ili kutetea haki za wasichana na kuziibua changamoto wanazokabiliana nazo duniani kote kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.
Pamoja na hayo pia Mei 28 dunia inaadhimisha siku ya hedhi safi na salama, mambo yanayolenga kufikia ulinzi kwa kuwaandaa wasichana na watoto wa kike wanaoingia kwenye umri balehe wasiachwe nyuma kwenye upatikanaji wa taulo za kike, ambazo pia upungufu wake unasababisha wengine washindwe kusoma.
Itakumbukwa kuwa maazimio ya mkutano huo , yalipokelewa, kuridhiwa na kusainiwa na serikali ya Rais Benjamin Mkapa, ambaye alianzisha michakato mbalimbali ya kuendeleza usawa wa kijinsia , kuwezesha na kushirikisha wanawake kiuongozi.
Akidumu na miaka 30 ya Beijing, astahili siku ya kuenziwa kitaifa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED