Dabi 7 Simba, Yanga zilizoota mbawa Dar

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:34 PM Mar 10 2025
Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama (katikati), pamoja na wachezaji wenzake ambao walifika uwanjani hapo juzi licha ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo huo
Picha: Mtandao
Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama (katikati), pamoja na wachezaji wenzake ambao walifika uwanjani hapo juzi licha ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo huo

MECHI ya 'Dabi' iliyokuwa ichezwe Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, iliota mbawa Jumamosi iliyopita baada ya kutokea mtafaruku wa watu wanaosemekana ni mabaunsa wa Yanga kuzuia msafara wa wachezaji wa Simba waliokuwa wanataka kuingia uwanjani kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo kwa mujibu wa kanuni.

Kutokana na kadhia hiyo, Klabu ya Simba iliandika barua Bodi ya Ligi kuelekeza kuhusu tukio hilo, ikieleza azma yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu ya kuzuiwa kutumia haki yao kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye kanuni 17:45 ya Ligi Kuu, kuhusu taratibu za michezo.

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), ikaamua kuahirisha mchezo wa dabi, baada ya kubaini uvunjifu wa kanuni ambayo iliizuia timu mgeni kufanya mazoezi kwenye uwanja husika ambao mechi inatakiwa kuchezwa.

"Kwa sababu pia bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeanisha matukio kadhaa yalioambatanishwa na tukio hilo la kuzuiwa basi la Klabu ya Simba na kuzuiwa kuingia kufanya mazoezi, huku baadhi ya matukio yakihitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, bodi kupitia kamati yake imeamua kuuahirisha mchezo huo kwa mujibu wa kanuni ya 34:1 (1.3), ya Bodi ya Ligi kuhusu kuahirisha mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitazosaidia kufanya maamuzi ya haki," ilisema taarifa hiyo.

Hili ni tukio la saba kwa michezo ya timu hizo kushindwa kufanyika kwa sababu mbalimbali, katika historia ya michezo ya dabi.

Katika mashaka haya, tumekusanya taarifa za michezo mingine ambayo iliota mbawa kwa kutofanyika...

Yanga vs Simba -1969

Ilikuwa ni Machi 3, 1969, wakati huo iliitwa Klabu Bingwa ya Taifa, mikasa nayo ilikuwa nimgi sana.

Simba ilicheza dhidi ya African Sports, baadaye ikabainika kuwa walimchezesha kipa wa timu ya Ujamaa ya huko huko Tanga bila kufuata taratibu. Mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1.

Simba ikakata rufaa wakitaka kupewa ushindi katokana na kosa hilo. Hata hivyo, African Sports, ilisema ilifuata taratibu zote na waliomba idhini ya FAT kumchezesha kipa huyo kutokana na kipa wao namba moja kupata maradhi ya macho. Na kweli FAT ilimruhusu, ingawa ilikuwa kimakosa kwani alikuwa ni kipa wa timu nyingine na ikakiri kuwa walikosea, na kudai watalishughulikia.

Kutokana na matatizo mengi ya utawala, serikali ilivunja uongozi wote wa muda wa FAT, ikaunda Kamati ya Muda ya kuendesha soka.

Barua ya Simba bado ilikuwa mezani kuomba ikitaka kupewa ushindi katika mchezo huo kutokana na wapinzani wao kuchezesha kipa asiyestahili.

Kamati ikairudishia Simba pesa ilizolipa kukata rufaa, hata hivyo haikuona umuhimu wa kuipa ushindi kwa madai kuwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

Simba ilitishia kuwa kama haikupewa ushindi haitocheza mchezo unaofuata dhidi ya Yanga na Machi 3, 1969. Ilionekana kama utani. Kama walivyoahidi, Simba haikutokea siku hiyo.

Kamati ya muda ya TFF, ikaipa ushindi Yanga wa mezani na kuitoza Simba faini ya shilingi 500 (mia tano), ambazo zilipaswa kulipwa kabla ya kuendelea na ligi, vingine haitocheza mchezo wowote.

Baada ya kuona hali inakuwa mbaya, viongozi wa FAT na wa serikali walikaa na kumaliza sakata hilo kwa kuondolewa faini Simba na kuruhusiwa kuendelea na ligi.

 Simba vs Yanga - 1992

Ulikuwa ni mchezo wa mzunguko wa pili, Ligi Daraja la Kwanza Bara, ambapo Yanga ilikataa kupeleka timu uwanjani kwa sababu tu tayari ilishatwaa ubingwa.

Yanga iliikwepa Simba katika mchezo uliokuwa upigwe, Septemba 26, 1992, kwa kile ambacho viongozi wao walidai mechi hiyo haikuwa na maana yoyote kwao kwa sababu tayari walikuwa wametwa ubingwa.

Simba ilipewa ushindi wa mezani wa pointi mbili na mabao mawili, Yanga ikipigwa faini ya Sh. 250,000, ambazo zililipwa na aliyekuwa mfadhili wao ambaye ndiyo kwanza alikuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Pan African, Murtaza Dewji.

Yanga vs Simba - 1996

Simba iligomea mchezo huo uliokuwa upigwe, Februari 26, 1996, kwa madai kuwa walikuwa wanajiandaa kwenda kucheza mchezo wa Kombe la Washindi Barani Afrika, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Chapungu Rangers ya Zambia.

Awali, Simba iliandika barua FAT kuhusu ombi lao hilo, lakini lilikataliwa. Simba ikagoma kucheza dhidi ya Yanga, ambayo ilipata pointi mbili na mabao mawili ya mezani. Cha ajabu ni kwamba Chapungu yenyewe nayo haikuja kucheza mechi dhidi ya Simba nchini. Simba ikapata ushindi wa bure na kuvuka hatua ikayofuata ya michuano hiyo ya kimataifa.

Simba vs Yanga - 2002

Yanga ilimsajili winga mwenye kasi wakati huo, Said Maulid kutoka Simba.

Siku chake baadaye, Wizara ya Mambo ya Ndani ikatangaza kuwa mchezaji huyo hakuwa raia wa Tanzania.

Taarifa hiyo ilitoka siku chache kabla ya mechi ya dabi, Julai 2002. Yanga walitaka mchezaji huyo aruhusiwe kucheza mchezo huo, lakini mamlaka ilikataa ikidai kwanza afuate taratibu zote kama mchezaji kutoka nje ya nchi, ikidaiwa alikuwa ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mchezaji huyo alifungua kesi mahakamani na kushinda, akarudishiwa uraia wake.

FAT iliahirisha mechi hiyo ambapo ilichezwa kipindi ambacho amesharudishiwa uraia.

Simba vs Yanga - 2008

Simba na Yanga zilitakiwa kucheza mechi ya kuwania mshindi wa tatu, Kombe la Kagame, Julai 27, 2008, baada ya timu zote kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo iliyokuwa ikichezwa hapa hapa nchini.

Yanga ikagoma kwenda kucheza, ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu wakati huo, Imani Madega (marehemu), alisema walikubaliana na Simba kugoma, lakini wenzao waliwasaliti.

Akasema awali walikubaliana na Shirikisho la Afrika Mashariki (CECAFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kwamba wapewe kiasi cha Sh. milioni 50 kabla ya mchezo huo, lakini hawakupewa, ndipo wao walipogoma.

Simba vs Yanga - 2021

Katika mchezo huu, Yanga iligomea mechi kutokana na mabadiliko ya muda.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kusogeza mbele mechi ya Ligi Kuu iliyokuwa ianze saa 11:00 jioni na kutakiwa kuanza saa 1:00 usiku, Klabu ya Yanga iligomea uamuzi huo.

Awali, TFF ilisema ilipokea maelekezo ya mabadiliko ya muda wa kuanza mchezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Yanga iliondoka uwanjani baada ya muda wa saa 11:00 kupita, baadaye ikatoka taarifa kuwa mchezo huo umeahirishwa.