UNAPOKUWA unapiga mswaki kila uchao, yapo yakufuatwa ingawaje inavyotakiwa kuwa, ndivyo sivyo, anafunguka bingwa wa tiba.
Hatua za kufuatwa zinashauriwa na wataalamu wa kinywa na meno, makundi yote yakiwamo watoto na wajawazito, kuna misingi ya kuzingatia inatajwa na wataalamu, pia miongozo ya afya.
Mswaki una ukomo wa matumizi na muda wa kupiga ni dakika kadhaa. Kusafisha pande zote za kinywa ni muhimu kuzingatiwa, ikiwamo kuusafisha ulimi.
Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno, Josephat Kunji, kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Epiphany, iliyopo Dar es Salaam, anatoa elimu hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kinywa na Meno Duniani.
Siku hiyo huadhimishwa kila mwaka Machi 20, huku hospitali hiyo ikifika katika Shule za Doris, Dar es Salaam, kuwapa elimu wanafunzi, ikiwamo walimu, walezi na wazazi wao.
“Unapozungumzia mswaki wa kijiti, ni mgumu na matokeo yake utaumiza fizi ambayo imezunguka meno, wengi huja fizi imelika, kukwaruzwa hasa ile ‘layer’ ya juu inakuwa imelika sana.
“Matumizi ya majivu, mkaa, sabuni, chumvi hazina madini ya ‘fluoride’ sio njia sahihi, kwa sababu itasababisha watu kuharibu meno. Pia, kwa mwaka uwe umebadilisha mara nne kwa mwaka, jamii ibadilike, utauona mswaki tu umeshakuwa mgumu. Badilisha.
Pia anasema wakati wa kusafisha kinywa, maji yasitumike muda huo huo baada ya kupiga mswaki, badala yake ipite dakika 15 hadi 30 kuruhusu floraidi ifanye kazi kwenye meno.
“Imezoeleka, ingawa si sawa kusukutua na maji kinywa baada ya kuswaki, hatua hiyo inaondoa floraidi haraka. Subiri zipite dakika 30 kisha urudi tena kusukutua au usisukutue.
"Wengi wanatumia dawa ambazo hazina madini ya floraidi, wengine wanatumia mkaa. wengine majivu na wengine hadi karafuu!
“Hizo zote sio namna ya kufanya meno kuwa masafi na kujikinga na wadudu wanaosababisha meno kuoza,” anasema Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo.
Anaendelea: “Mtu anapopiga mswaki, anatakiwa atumie dakika mbili baada ya hapo anatema povu na asiweke maji mdomoni.
“Unapopiga mswaki na kuweka maji mdomoni ukasukutua na kutema unakuwa umetoa dawa ambayo ilikuwa muhimu kwa meno kuoza.’
Bingwa huyo anasema, kwa upande wa matumizi ya dawa za asili za meno anasema, mfano kutumia karafuu kunapunguza tu maumivu na haitibu, hivyo maumivu yatapungua, lakini madhara yake ni makubwa.
"Jino litaendelea kuoza hadi kwenye kiini na jino kutengeneza jipu linalotoa usaha ambapo ule usaha ni hatari inaweza ksababisha mtu kufa.
"Wapo wanatumia hadi mafuta ya betri ya gari wengine ya tranfoma wanaweka kwenye jino hizo njia ya matibabu sio nzuri unatuliza tu maumivu hujatibu tatizo,” anasema.
Anafafanua kuwa, wakati wa kupiga mswaki, mtu asiteme dawa iliyomo mdomoni dakika chache tangu kuanza kuswaki, bali afuate hatua ya kuanza kupiga mswaki meno ya juu pande zote mbili, kisha pande mbili za chini na hatimaye ulimi.
“Unaposafisha ulimi anzia nyuma kuja mbele, ukianzia mbele kwenda nyuma, uchafu utaurudisha ndani na hata kuumeza. Ukiswaki usisukutue na maji, acha dawa ya meno yenye floraidi kwa dakika kadhaa,” anasema bingwa huyo.
Anashauri wakati wa kupiga mswaki, ni vyema kusukutua kwa maji safi hasa yaliyotibiwa au kuchemshwa kwa sababu unaweza kuyameza na kuhatarisha tumbo lako.
Mtaalamu huyo anashauri jamii kubadilika, kwamba dawa ya jino sio kung'oa, bali ni kufanya matibabu sahihi kulingana na tatizo lililopo, unaweza kuziba kawaida na kukata mzizi wa jino na hatua mwisho kabisa ni kung'oa.
KUTOKA WIZARANI
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, akizungumza na gazeti hili katika kuadhimisha siku hiyo, mwaka huu, anasema kutunza kinywa na meno, ratiba ya kupiga mswaki ni mara mbili kwa siku, ingawa:
“Usipige mswaki meno yako mara baada ya kumaliza kula chakula, subiri kwanza kwa dakika 30, kuepusha kuyaumiza meno na kukwangua gamba gumu la nje la jino,” anasema.
Anasema, matumizi sahihi ya kiwango cha dawa ya meno kwenye mswaki, kabla ya kuswaki kinywa ni chanzo cha kuyakinga dhidi ya kuoza na kutoboka.
Ubora wa dawa za meno zenye madini ya floraidi, unatajwa kuongeza ulinzi wa meno kwa kuyakingà kutooza.
Anasema ili kujikinga na meno kuoza, inashauriwa kupiga mswaki meno mara mbili kwa siku (asubuhi na usiku kabla ya kulala), kwa kutumia dawa yenye madini ya floraidi iliyo na ubora.
“Kuanzia jino la kwanza linapoanza kuota na hadi miaka miwli, weka dawa ya meno kwa ukubwa wa punje ya mchele (900-1000 ppmF- Dawa ya meno maalumu kwa watoto).
Kwa wenye miaka mitatu hadi mitano, weka dawa ya meno kwa ukubwa wa punje ya harage 9900-1000 ppmF-Dawa ya meno maalumu kwa watoto)
Miaka sita mpaka umri wa mtu mzima weka dawa ya meno ijae eneo lote la brashi ya kwenye mswaki (1400-1500 ppmF- Dawa ya Meno ya watu wazima),” anasema Dk. Nzobo.
HALI YA TIBA
Mkurugenzi Dk. Nzobo, anasisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi kwamba, matumizi sahihi ya dawa ya meno na yenye kiwango cha ubora wa madini ya floraidi, ni pamoja na ujazo wa kila siku, huondoa athari hasi kwa kinywa.
Anaeleza kwamba kiwango cha wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya kinywa na meno nchini inakua, huku kipindi cha kuanzia Julai, mwaka 2023 hadi Juni, mwaka huu, watu 535,324 waliohudhuria kwenye vituo vya kutoa matibabu nchini, walibainika kuoza meno.
Kati yao, wagonjwa 219,482 sawa na asilimia 41, walifanyiwa matibabu ya kuziba jino (kutibu jino), kwa kuziba kwa dawa ya kudumu; kuziba kwa dawa ya muda na kutibu mzizi wa jino (Root Canal Treatment).
Lengo kuu la serikali kupitia Wizara ya Afya, ni kuhakikisha inaweza kutibu meno ya watu kwa asilimia 60 na siyo kuyang’oa.
Kabla ya uwekezaji huo mkubwa unaofanywa na serikali, miaka ya nyuma tulikuwa tunaziba kwa asilimia mbili na kung’oa watu meno kwa asilimia 98.
Kwa sasa mambo yamebadilika na yatazidi kuwa bora zaidi mpaka lengo la kuziba kwa asilimia 60 litakapofikiwa ndani ya muda mfupi.
Hospitali za rufaa za mikoa zinazoziba meno watu wengi kuliko kung'oa ni 23 nchini, ikiwamo Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH).
Zingine zenye hadhi ya rufani kimkoa ni Mawenzi, Mt. Meru RRH Njombe, Simiyu, Mwalimu Nyerere Memorial, Temeke, Songwe, Singida, Manyara, Iringa, Geita na Bukoba.
Kadhalika, kuna Amana, Morogoro, Dodoma, Seko Toure, Sumbawanga, Tanga, Sokoine, Shinyanga, Maweni na Shinyanga.
Dk. Nzobo anazitaja pia hospitali za wilaya 38 nchini zinazoziba meno (kuyatibu) kwa wingi kuliko kuyang'oa ni Makambako, Arusha, Bagamoyo, Bariadi, Bukombe, Chato, Frelimo na Geita.
Zingine ni Hai, Handeni, Igunga, Ikungi, Kalambo, Karagwe, Kigamboni, Kiomboi, Kondoa, Korogwe, Kyela na Mahenge.
Pia anataja hospitali za: Mbarali, Meru, Misungwi- Iteja, Monduli, Mtowisa, Muheza, Ngorongoro, Nsimbo, Nzera na Rombo, Rorya DC na Siha.
“Kadhalika, hospitali Singida, Tanganyika, Tukuyu, Uvinza, Wanging'ombe na Vwawa. Tanzania bila vibogoyo au watu wenye mapengo inawezekana,” anahitimisha mkurugenzi huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED