WATETEZI wa haki za mtoto wa kike wanawanyooshea kidole wabunge kwa kushindwa kumtetea, anayekandamizwa na Sheria ya Ndoa.
Aidha, wanakosolewa hawakusimamia uamuzi wa mahakama wa kuitaka serikali ibadilishe vipengele vya sheria hiyo ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa chini ya miaka 18 kuozwa.
Watetezi wanawaona wabunge wanaomaliza muhula wao wa miaka mitano mwaka huu kuwa hawakusimamia maendeleo ya mtoto wa kike kwa kutosimama na maamuzi ya mahakama iliyotaka asiolewe chini ya miaka 18.
Profesa Ruth Meena, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Wakfu wa Mfuko wa Wanawake (WTF), pia mwanaharakati masuala ya usawa wa kijinsia, anayesema kuna mila, taratibu na sheria zinazoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri mdogo.
“Pamoja na kwamba Mahakama ya Rufani, ilibatilisha sheria hiyo, bado wabunge wetu wanasita kuipitisha kwa madai kwamba ni suala tete, linalogusa tamaduni na mila za Watanzania wengi, hivyo kwa hali ambayo haikuwa ya kawaida, bunge likarudisha suala hili kwa wananchi ili kuendeleza mjadala,” anasema.
Profesa Ruth ambaye pia ni mwanazuoni mstaafu wa fani ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema uamuzi huu haukukinzana tu na dhana ya mgawanyo wa mamlaka ya mihimili ya dola, lakini unaibua maswali mengi kuhusu uwakilishi wa Watanzania na utetezi wa haki za wanyonge.
Anawataja watoto ambao hawana uwakilishi bungeni, wabunge waliotarajiwa kuwawakilisha hawakusikiliza sauti yao.
“Hatua iliyochukuliwa inamaanisha kwamba mtoto wa kike hana ulinzi wa kisheria, anapolazimishwa kukatisha masomo na kuoezwa, ili mradi aidha wazazi,walezi au mahakama imeridhia, hapa panajitokeza maswali mengi,’’anasema Profesa Ruth.
Anahoji, wale wote wanaodai kwamba kumekuwa na msisitizo mkubwa mno kuwatetea watoto wa kike na kuwaacha nyuma watoto wa kiume, wamepitia hoja za mahakama iliyotaka kuzingatiwa haki za mtoto wa kike?
“Je,watetezi wa mfumo dume, wametambua jinsi gani sheria kandamizi zinavyoendelea kumbagua mtoto wa kike? Je kusitisha au kuahirisha hukumu ya Mahakama ya Rufani kama chombo cha utoaji haki, ni kuhalalisha mfumo kandamizi wa kisheria dhidi ya mtoto wa kike.
“Kwa uamuzi ule wa bunge, ni mtoto wa kike au wa kiume aliyepokonywa haki zake? Watetezi wa haki za mtoto wa kike, wasikatishwe tamaa waendelee kupaaza sauti,kufanya hivyo hakuna madhara kwa mtoto wa kiume,” anasema.
NDOA NI NINI?
Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya 1971, ni makubaliano ya hiari kati ya watu wawili mwanamke na mwanaume.
Hapo ndipo inaibua swali, iweje mtoto wa kike alazimishwe kuolewa akiwa na umri mdogo kwa idhini aidha wazazi au walezi, hata ya mahakama? Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inatafsiri ‘mtoto kuwa ni mtu aliye chini ya umri wa miaka 18”.
Anasema, hukumu ya Mahakama ya Rufani ililenga kusahihisha suala hili ambalo limebakia ndani Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kwa kuruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa mdogo.
“Ndoa za utotoni zinaathiri vipi haki za mtoto wa kiume, ambaye yeye halazimishwi kuoa katika umri mdogo? Utetezi wa mtoto wa kike ambaye ndiye analazimishwa kuolewa katika umri mdogo na unaathiri vipi haki na uwezo wa mtoto wa kiume,” anasema,
Katika mazingira hayo, mtoto wa kike anapolazimishwa kuolewa katika umri mdogo, wa kiume anapokonywa haki au uwezo gani? Kinyume chake, ni mtoto wa kike ndiye anayepokonywa haki yake ya kukua, kupata elimu, kuwa na afya bora na kupata hifadhi ndani ya jamii yake.
“Mbaya zaidi, mtoto wa kike huyu haolewi na mtoto mwenzake wa kiume, bali anaozwa kwa nguvu kwa mtu mzima – wengine wakiwa watu wenye umri wa baba au babu zao,” anasema.
Watoto hao hulazimishwa na wazazi au walezi kuingia kwenye ndoa ili wazazi wapate mahari, wanapitia mateso makubwa kwenye ndoa hizo, wanakatishwa ndoto za kuhitimu masomo yao, ndoto za kufikia uwezo wao na kukuza vipaji vyao. Wanaishi katika ukatili, wanaathirika kisaikolojia, wanapata madhara ya kimwili, ulemavu na hata vifo.
Takwimu zinaonyesha kwamba theluthi moja ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-18 walishaolewa kabla ya kufikia miaka 18.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania(JUKATA) Dk. Ananilea Nkya anawaambia wahariri wa vyombo vya habari hivi karibuni kuwa ni jambo linaloumiza kuona kwamba jamii haijaelewa chimbuko la kumwezesha mtoto wa kike, hivyo washiriki kutoa elimu ili kufanikisha ukombozi wa mtoto huyo.
Dk.Ananilea ambaye pia ni mwanahabari mkogwe anasema wanahabari wana jukumu kubwa la kuielimisha jamii jinsi ambavyo mfumo dume umekandamiza haki ya mtoto wa kike.
“Wahariri ndiyo waamuzi wa kuona habari ipi inapaswa kupewa uzito, ni vyema kuandaa agenda pamoja na kuonyesha historia jinsi mfumo dume ulivyojenga ubaguzi kwa mtoto wa kike na kukwamisha maendeleo yake na jamii kwa ujumla,”anasema.
Anasema habari ambazo zitaonyesha jinsi gani wabunge wengi waliotegemeo walivyokwama kumtetea mtoto wa kike kwa kupinga ndoa katika umri mdogo, hivyo wananchi wawapime kama wanastahili kupewa nfasi ya kurudi tena bungeni, hivyo watumie kura zao vyema kuwadhibiti.
Hata hivyo kuna baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakionyesha jitihada za wazi za kuangaika kufanikisha marekebisho ya sheria ya ndoa wakionyesha kuusubiri muswaada husika na kukumbusha ufikishwe bungeni.
Oktoba 14, mwaka jana Nipashe iliripoti taarifa za mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima, kuomba Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, kupeleka bungeni muswada wa kurekebisha Sheria ya Ndoa.
Sima anataka marekebisho hayo ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, anatoa kauli hiyo akiwa jijini Dar es Salaam.
Ni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yakiandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) na kushirikisha wasichana na wadau kutoka mikoa mbalimbali.
Sima anabainisha kuwa ndio wakati mahususi kwa wizara hizo za kisekta zinazohusika katika eneo hilo, kufanyia kazi sheria hiyo.
"Kazi kubwa ya wabunge ni kushauri serikali, nitoe wito sasa kwa mawaziri wa kisekta, huu ndio wakati wa kutuletea muswada, tuchakate, upelekwe bungeni na wabunge wapate nafasi ya kuchangia, kupata mawazo mbadala ili jambo hili litekelezeke.
Anaeleza kuwa kuna utata kuhusu umri sahihi wa mtoto wa kike kuolewa, tunaona Mtandao wa Elimu Tanzania na wadau wengine wameamua kwa dhati kuleta chachu ya mabadiliko ya kutaka mtoto wa kike atimize ndoto yake, wakihamasisha ulinzi dhidi ya ukatili na unyanyasaji.
Aidha, Mei mwaka jana Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini, anaeleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria imekamilisha maandalizi ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kwamba taratibu zinaandaliwa za kuufikisha bungeni kwa kujadiliwa kisha kupitishwa kuwa sheria.
Sagini anayasema hayo bungeni akijibu swali la Dk. Tea Ntara (Mbunge Viti Maalum), akitaka kujua lini serikali italeta muswada wa Sheria ya Ndoa ili iendane sambasamba na vita dhidi ya ndoa za utotoni.
Sagini akijibu hoja anasema mandalizi muswada yanafanywa ikiwamo kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuanzia wazee wa kimila, viongozi wa kidini, wanafunzi wa ngazi,wabunge na wabobezi wa taaluma yatakayoondoa ubishani wa umri upi sahihi wa kuolewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED