MPANGO MAENDELEO SHULE SALAMA...Ofisa Elimu: Umewaingiza mabinti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:10 PM Mar 26 2025
Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, akifafanua jambo. Aliyekaa ni, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Aisa Rupia
Picha: Mtandao
Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, akifafanua jambo. Aliyekaa ni, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Aisa Rupia

HADI sasa nchini, mikakati ya elimu shuleni inaendeshwa chini ya vivuli vikuu viwili; Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), zote zilianzishwa katika zama serikali awamu ya pili.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hivi sasa ina kinachoitwa ‘Mpango wa Shule Salama katika shule za sekondari, pia za msingi.

Hoja ni kuhakikisha elimu inaboreshwa kwa kiwango cha juu zaidi, ikipiga vita angalizo la kihistoria “kukabili ujinga na umaskini” kwa jamii.

Mkoani hapa, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Aisa Rupia, anasema Mpango wa Shule Salama uko ndani ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Shule za Sekondari (SEQUIP).

Anafafanua kwamba, ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/21/22, akiutaja ni wa miaka mitano, mradi ukiendeshwa na serikali, kwa fedha zitokanazo na mkopo wa Benki ya Dunia (W0RD BANK)

Rupia anaeleza kuwa mpango huo umehusisha jamii na kuanzisha chombo kimoja kinachoitwa, Umoja wa Wanafunzi, Wazazi na Walimu (UWAWA) ukijihakikishia mambo kadhaa.

Hapo anayataja kuwa ni wanafunzi kupata mahitaji yao ya msingi, kuwa na jamii iliyoelimika, kuzuia ukatili kwa watoto na jamii kuhakikisha wanafunzi wanamaliza mzunguko wao wa elimu shuleni.

Ni mfumo unaohusisha maofisa maendeleo na ustawi wa jamii, polisi maofisa watendaji kata na viongozi wa bodi katika kata zote.

Hiyo anaitaja kuwa hatua ya utekelezaji ulioanza kwa shule za sekondari 48 zenye watoto wenye mazingira magumu na sasa unatekelezwa katika shule zote 357 za sekondari mkoani Mwanza.

Staili ya utekelezaji wake, anataja ni kwa wanafunzi kubadilishana mawazo kuhusu stadi ya maisha yao, wakitoa maoni yao, kwenye masanduku ya maoni shuleni kupitia umoja wao.

Vilevile katika wajihi huo wa maendeleo, Rupia anasema shule zote zimebuni bustani za mboga na mashamba ya kulima mazao ya chakula.

Utaratibu uliopo, ni kwamba asubuhi wanafunzi hupatiwa kifungua kinywa cha uji na mchana wanakula, akitaja Sera ya Elimu kwa sasa haitaki wanafunzi kusoma wakiwa na njaa shuleni, hivyo  wazazi nao ni sehemu ya mchango wa mahitaji muhimu kuleta ufanisi katika sekta hiyo.

Kupitia mpango huo, anasema hivi sasa malalamiko ya ukatili waliokuwa wakipokea kila mara ofisini, yamepungua, ufaulu nap umeongezeka kwa wanafunzi kidato cha nne, tofauti na zamani walipokuwa hawajafikiwa na mradi huo wa SEQUIP 

Rupia anataja changamoto zao kubwa, ni ugumu wa jinsi ya kuyafikia makundi mbalimbali yaliyo katika mapito kimaisha, hata wakaya elimu ya shule salama kama vile madereva wa daladala, bodaboda wasiendelee kuwabeba wananfunzi mishikaki.

MALENGO MATATU

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, anaeleza kuwa Mpango wa shule salama, unaoratibiwa chini ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Shule za Sekondari umeleta mafanikio makubwa zaidi katika sekta ya elimu mkoani hapa.

Nkwabi anataja malengo yao makubwa matatu, ni kuboresha elimu shule za sekondari mkoani, kuongeza fursa kwa watu wengi kupata elimu ya sekondari, kuwezesha ukarabati, kupanua shule za zamani, kujenga mpya, kujenga mabweni na maabara.

Anasema lengo la pili ni kuhakikisha mazingira salama kwa wanafunzi wa kike wanapokuwa shuleni, ikiwa lengo la tatu kuzuia mdondoko kila mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza, aweze kumaliza kidato cha nne na kidato cha tano ahitimu kidato cha sita.

Vilevile kuna malengo mawili ndani ya mpango huo, ambayo ni kuhakikisha nafasi bora kwa wasichana, kuzuia mdondoko ili kumaliza mzunguko wa elimu shuleni.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu huyo, hadi sasa sekta yao imejikita kutoa elimu ya kila siku kwa wanafunzi na walimu shuleni kuhusu Mpango wa Shule Salama.

Anafafanua kuwa, sekta ya elimu imeweka kigingi kupitia mpango huo kwa wanafunzi na walimu shuleni, kukomesha tabia za wanafunzi kupigana, kunyang’anyana mabegi, kuibiana darasani vifaa vya shule na walimu kutotoa adhabu mbaya zinazochangia baadhi yao kuacha shule.

Kutokana na mafanikio hayo, anataja serikali imejenga shule za sekondari za kutosha kila mkoani Mwanza, zenye nafasi bora kwa wasichana na wavulana.

Nkwabi anasema, lengo lililoko ni kuondoa utoro anaoutaja ‘rejareja’ na ‘sugu’, ikiwamo asilimia 60 ya utoro shuleni unaosababishwa na mambo kama umaskini katika jamii.

Nkwabi anasema kuna mazingira ya wazazi nao wamejijengea kuwa chanzo utoro kwa watoto, kwa sababu ya kuwatumia kama sehemu ya uchumi kutokana na kuwapa shughuli za uzalishaji.

Anazitaja baadhi yake ni kuuza samaki mtaani, maandazi na kufanya kazi za majumbani, kilimo, kuuza mighahawa, watoto kufiwa wazazi wao na kuleana wenyewe.

Pia, kuna jamii ya wavuvi na wafugaji anayieleza haiwathamini watoto wao wa kike hata wa kiume kupata elimu sahihi, kwa sababu ya kufanya kazi za ndogo za uvua samaki na kuchunga ng’ombe, wengine wakiuguza wazazi wao ambao ni wagonjwa.

Nkwabi anasema sekta ya elimu ina sheria ya lazima katika shule za sekondari, kuhusu wanafunzi watoro, ambayo inasimamiwa na walimu wakuu, watendaji wa kata,vijiji,mitaa na vitongoji.

Anataja wajibu wa mwalimu mkuu ni kupeleka orodha ya watoto watoro kwa viongozi hao ambao wanawajibu wa kuchukua hatua kisheria na kuwarudisha shuleni.

Wazazi wanaohama sehemu moja kwenda nyingine, anasema wanatakiwa kuomba uhamisho wahame na watoto wao.

Lingine analitaja kuwa na uzazi mkubwa anaitaja kuwa sababu moja wapo ya umaskini, hata wanashindwa kuwasomesha shule katika namna stahiki.

Mustakabali mwingine anaoutaja Ofisa  Elimu Nkwabi, ni namna ya kudhibiti utoro uliokuwa ukisababishwa na shule, walimu kutoingia darasani kufundisha nao umepunguzwa.

Anautaja Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umewavuta kiutendaji kwa kupunguza umaskini katika jamii ya mkoani hapa.

Mkoa wa Mwanza mwaka 2020, anataja kiwango cha utoro klikuwa asilimia 11, lakini sasa anataja iko katika asilimia tatu pekee.

Nkwabi anasema kwa wanafunzi ambao hawamalizi mzunguko wa elimu shuleni, mafanikio kwa upande wao uko kupitia makakato huo wa miaka mitano wanaouendesha.

MIMBA SHULENI.

Kuhusu wanafunzi wanaopata mimba shuleni, sheria inawaruhusu kwenda kujifungua, baada ya miaka miwili mwanafunzi anarejea shuleni kuendelea na masomo. 

Nkwabi anataja utaratibu ulioponi kwa mwanafunzi huyo anarudia kidato alichokuwa wakati akipata ujauzito, akiwa huru kuhama, iwapo atapenda

Anasifu haina madhara kwao kwa kwa wanafunzi wengine darasani, akisema lengo la utaratibu huo unamhakikishia mwanafunzi kupata elimu yake, huku ikimuokoa mtoto aliyezaliwa, naye baadaye aweze kupata elimu.

Hapo anaitolea tafsiri kwamba, iwapo mama mzazi akikosa fursa ya elimu, kuna uwezekano mtoto kuangukia mstari huo, taifa linazalisha kundi kubwa la wajinga.

Anasema, wanafunzi hao hupewa ushauri nasaha shuleni, wakifundishwa dhana ya maadili.

''Katika mkoa wa Mwanza, jumla ya anafunzi 71 wa kidato cha nne shule za sekondari waliopata mimba na kurudi shule mwaka jana, baada ya kujifungua wamefaulu wote, kuendelea na kidato cha tano,” anasema Nkwabi:

Anabainisha ufaulu wa kidato cha pili mwaka juzi mkoani humo ulikuwa asilimia 80; mwaka jana 2024 umepanda hadi kufika asilimia 87.

Pia, anataja katika kidato cha nne mwaka juzi ulikuwa asilimia 89 mwaka jana umewekwe kufika asilimia 98, sasa wanajisifia mafanikio hayo.

ADHABU VIBOKO

Kuhusu adhabu ya viboko, Nkwabi anaieleza kuwa bado haijafutwa shuleni, akinukuu iko kwenye Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978.

Ndani yake inataja kiwango cha juu cha adhabu ya viboko kwa mwanafunzi atachapwa hadi viboko vinne, katika shule zote za sekondari na msingi, mwanafunzi wa kiume atachapwa makalioni na wa kike kiganjani. 

Anasema mwalimu mtoa adhabu atatia saini jina lake na taarifa za adhabu, muda aliotoa adhabu, aina ya adhabu na kosa.

Hapo Ofisa Elimu Nkwabi, anataja tahadhari zake ni kutumia nyenzo kama rungu, fimbo za miba, kuchapa kichwani au sehemu nyingine ya mwili wa mwanafunzi hairuhusiwi kisheria.

Pia, anaeleza kuwapo adhabu mbadala aina nyingi, kama kufagia au kulima bustani ni sehemu mojawapo.