ZAIDI ya theluthi ya wanawake wanaofanya kazi duniani wameajiriwa katika miradi ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Wana majukumu mengi kama uhifadhi, usafirishaji, usindikaji na usambazaji, linasema Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Lakini FAO, inaongeza kuwa kukosekana kwa usawa wa kijinsia mfano kuwepo fursa ndogo kwa wanawake kupata ujuzi na ŕasilimali kwenye karibu sekta zote, husababisha pengo kubwa la uzalishaji kati yao na wanaume wakulima mashambani.
Hali ilivyo duniani si tofauti na Tanzania, kwa kuwa suala la umiliki wa ardhi kwa wanawake halijakaa sawa, licha ya kwamba ni rasilimali muhimu kwenye uzalishaji, baadhi ya makabila wanawake hawaruhusiwi kurithi ardhi.
Jumamosi Marchi 8, ni kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, kikifanyika kitaifa Arusha, hata hivyo, kama ilivyo sehemu nyingine duniani, visiwani Zanzibar kinamama walio katika sekta ya kilimo wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo umiliki wa ardhi.
Salma Shija Masanja (47) mkulima kiongozi katika Kijiji cha Bungi mkoa wa Kusini Unguja, anasema licha ya kulima kilimo mseto eneo analolima si lake.
Anasema ameazimwa hivyo huishia kulima mazao ya muda mfupi ikiwemo mboga na matunda na hawezi kufanya kitu kingine, mwenye ardhi amemwambia nisilime mazao ya muda mrefu ili atakapolihitaji kusiwe na vikwazo.
Salma mama wa watoto wane, anasema mabadiliko ya hali ya hewa, uwepo wa ua kali vinaathiri kilimo na kupunguza mavuno kutokana na ukosefu wa maji.
“Wanawake tunapambana kujikwamua kiuchumi lakini jua kali linatukatisha tamaa maana bila ya maji mimea haistawi, ”anasema.
Sekta ya kilimo inatajwa kuajiri takribani asilimia 35 ya Wazanzibari huku zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wakitegemea sekta hiyo kujikimu kimaisha.
Wakulima wanawake Zanzibar wamejua siri ya kuongeza mapato shambani kuwa ni kuongeza uwezo wa shamba kwa kulima mimea mbalimbali ambacho ni kilimo mseto.
Sabra Abdi (37), mkulima wa Kijiji cha Bungi, anasema ili kufanikisha kilimo mseto elimu kwa wakulima wanawake inahitajika kwa na kupatiwa pembejeo mbolea na vifaa vya kilimo.
Anasema baada ya kupata elimu wameunda kikundi na kuotesha miti ya matunda mbalimbali pamoja na viungo ikiwamo mdalasini miti 10,000, michungwa 1,160, miembe 910 na mafenesi 390.
Anaongeza kuwa licha ya kutokuwa na maeneo ya ardhi ya uhakika kwa ajili ya kilimo lakini malengo yao ni kujiendesha kimaisha kupitia kilimo ili kujikimu kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Wanatarajia kugawa miti mingi kwa wakulima kijijini hapo ili kuotesha na kupambana na athari za kimazingira ikiwamo mabadiliko ya tabianchi na kujiongezea mapato, anafafanua.
Aidha, kilimo hicho kimewanufaisha wanawake kwa sababu awali kabla ya kupata elimu kupitia mradi wa Zanzibar Women Leadership in Adaptation (Zan Adapt), walilima bila kuwa na utaalamu.
Kupitia mradi huo wamejifunza jinsi ya kutunza shamba na kupanda miti ya matunda kwa mpangilio maalum, kuitunza, kuifuatilia na kuisimamia anaeleza Sabra.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)-Zanzibar Dk. Mzuri Issa, anasema zile zama za kuwaachia kila kitu wanaume zimepitwa na wakati kwa sababu thamani ya ardhi imeongezeka na wanawake wanatakiwa kuitumia kujiimarisha kiuchumi na kupambana na umaskini.
Mkurugenzi mzuri anawataka wanawake vijijini kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za kiuchumi na umiliki wa ardhi, zinazotolewa na serikali kwa sababu watakapokuwa na umiliki watakuwa na uhakika wa kuendeleza kilimo.
Anaongeza kuwa TAMWA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilitekeleza mradi wa kuwahamasisha wanawake kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo, kiuchumi na biashara.
Anasema hiyo ni fursa muhimu ambayo wanawake wanatakiwa kuitumia kikamilifu kuona wanamiliki ardhi kwa shughuli za maendeleo na kiuchumi ili kuondokana na tabia za tegemezi kwa waume.
Ofisa teknolojia ya uzalishaji wa mradi wa Zan Adapt, Shabani Peter, anasema kupitia mradi huo wanalenga kuwafikia wakulima 4,000 na kati ya hao asilimia 80 ni wanawake ili kuwapa elimu na mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwamo kujikita kulima na kupanda miti.
Peter anasema mradi huo zaidi unalenga wanawake kwa sababu ndiyo waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi, wakitambua namna ya kukabiliana nayo na wakiwa na vipato itakuza uchumi na kuhifadhi mazingira.
Anasema lazima wawafundishe wakulima mbinu bora za kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa, kulinda, kuhifadhi udongo na unyevu unyevu pia.
Anasema miongoni mwa mbinu hizo ni kuhamasisha kilimo mseto ambacho kinaendana na mabadiliko ya tabianchi na kinachangia kupatikana mvua lakini pia ni kupanda miti.
Ofisa huyo, anabainisha kuwa kilimo mseto kimekuwa suluhisho muhimu kwa wanawake visiwani Zanzibar.
"Kilimo mseto si tu kwamba kinaongeza tija kwa wakulima, bali pia kinahifadhi mazingira kwa kupunguza matumizi ya kemikali hatarishi. Wanawake sasa wanajifunza mbinu hizi na kuzitumia mashambani," anasema Peter.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo sekta ya kilimo inayojumuisha mazao, mifugo na maliasili za misitu ni tegemeo kwa uchumi wa Zanzibar na inachangia moja kwa moja kwa wananchi kujikimu kimaisha.
Waziri wa wizara hiyo Shamata Shaame Khamis, anasema serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wakulima kupata elimu na teknolojia bora ili kilimo kiwe na tija na kukuza uchumi.
Anataja faida za kilimo mseto kuwa kinazuia mmomonyoko wa udongo, kuimarisha rutuba ya ardhi, kudumisha au kuboresha hewa ukaa ya udongo, ambayo hupunguza kutoa gesi chafuzi.
Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984, inatamka kuwa wanawake wanayo haki sawa na wanaume katika kumiliki ardhi kwa matumizi mbalimbali yakiwamo ya kilimo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED