URAIA PACHA; Haki ya asili, urithi nasaba, fursa maendeleo ya taifa -2

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:05 AM Mar 05 2025
Waziri wa  Katiba na  Sheria Dk. Damas Ndumbaro
Picha: Mtandao
Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro

KATIKA dunia inayoendelea kuunganishwa kwa kasi, mjadala wa uraia pacha unaendelea kushika kasi nje na ndani ya Tanzania.

Wakati baadhi ya watu wanapinga dhana hii kwa hoja za kihistoria au kiusalama, kuna haja ya kutazama kwa jicho la kisasa zaidi.

Wiki iliyopita tulitazama sehemu ya kwanza ya makala hii, sasa tuendelea na kipengele kingine muhimu kuhusu mjadala wa kuwa na hati za uraia na za kusafiria za mataifa mawili tofauti. Kwa kuanza na fursa zinazoibuka.

FURSA TANZANIA

Faida za kiuchumi, kitaalamu na kijamii za uraia pacha kwa Tanzania. taifa likiwa na diaspora kubwa barani Ulaya, Amerika, Mashariki ya Kati na Asia, linaweza kufaidika kwa kiasi kikubwa ikiwa litaruhusu uraia pacha kwa raia wake wa nje.

Manufaa yake ni pamoja na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja (FDI): Watanzania waishio nje wana mitaji mikubwa na wangependa kuwekeza nyumbani bila vikwazo vya uraia.

Aidha, kuboresha sekta ya elimu na afya , diaspora ya Tanzania ina wataalamu wengi wa tiba, uhandisi na teknolojia ambao wangerejea kusaidia maendeleo ya nchi.

Kuongeza mapato ya serikali ni faida kwani  Watanzania wa diaspora wakiruhusiwa kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa nchi, serikali itapata mapato kupitia remittance, kodi na ada mbalimbali 

AIdha, kuimarisha diplomasia ya kiuchumi., Watanzania walioko nje wanaweza kuwa mabalozi wa biashara na kusaidia kutangaza fursa za kiuchumi za Tanzania kwa wawekezaji wa kimataifa.

 Kuchochea uhamishaji wa maarifa na teknolojia, ni faida nyingine, diaspora ina ujuzi wa kisasa unaoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya viwanda, kilimo cha kisasa, na ubunifu wa teknolojia ndani ya nchi.

FAIDA KIUCHUMI

Uraia pacha katika dunia ya sasa, mtiririko wa watu, maarifa, na mitaji unahamasishwa kwa ajili ya maendeleo. Watanzania wengi wanaoishi nje wamefanikiwa kifedha, kielimu, na kiteknolojia, lakini wanashindwa kuwekeza kikamilifu nyumbani kwa sababu ya vikwazo vya kisheria vinavyotokana na kupokonywa uraia wao wa Tanzania.

Nchi kama Ethiopia na Rwanda zimepitisha sheria za kuwawezesha raia wao wa zamani kuwekeza kwa urahisi bila masharti magumu ya uraia.

Matokeo yake, zimeona ongezeko kubwa la uwekezaji kutoka kwa diaspora. Kwa mfano, Ethiopia imekuwa moja ya nchi zinazoongoza kwa kupokea fedha kutoka kwa raia wake wa nje, kiasi ambacho kinachangia zaidi ya asilimia tano ya pato la taifa.

Tanzania pia inaweza kufaidika na mtaji wa Watanzania waishio nje kwa kuwaruhusu kuwa na uraia pacha. Kwa sasa, Watanzania wengi walio na uraia wa nchi nyingine wanakumbana na vikwazo vya kisheria wanapotaka kumiliki ardhi, kuanzisha biashara, au kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Uraia pacha utahamasisha uwekezaji wa moja kwa moja kutoka kwa Watanzania walio nje na kuongeza mchango wao kwenye uchumi wa nchi.

DIPLOMASIA KIUCHUMI

Serikali ya Tanzania inajitahidi kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na kushirikiana na mataifa mbalimbali katika biashara na maendeleo. Hata hivyo, inaposhindwa kuwawezesha raia wake walio nje kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa nyumbani, inajikosesha fursa kubwa ya maendeleo.

Kwa mfano, China imekuwa na sera madhubuti ya kushirikisha diaspora yake katika maendeleo ya nchi.

Wachina waishio nje wamechangia sana kuinua uchumi wa nchi yao kupitia uwekezaji wa moja kwa moja, ushauri wa kitaalamu, na kuunganisha biashara za China na soko la kimataifa.

Tanzania inaweza kutumia mfumo kama huu kwa kuruhusu uraia pacha na kuweka mazingira rafiki kwa Watanzania waishio nje kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Kwenye suala la uraia pacha, tunahitaji hoja za kisayansi, kifalsafa, kimantiki na kitafiti, si hoja za kihistoria pekee.

Katika mjadala huo, Waziri wa  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi , anapinga suala hili kwa kutumia hoja za kihistoria, akirejea matukio ya zamani bila kutoa uchambuzi wa kisasa unaozingatia mazingira ya dunia ya sasa na changamoto zake. 

Tunamheshimu Prof. Kabudi kama msomi mwenye heshima kubwa katika taaluma ya sheria na diplomasia, lakini kama kweli tunataka kufanya maamuzi ya msingi kwa taifa letu, ni lazima mjadala huu uendeshwe kwa hoja za kisayansi, kifalsafa, kimantiki na kitafiti, badala ya kushikilia historia iliyopitwa na wakati.

UPINZANI URAIA PACHA

Uraia pacha na hoja dhidi ya upinzani wake, mtazamo wa kifalsafa na kimantiki. Katika mijadala kuhusu uraia pacha, kuna hoja zinazoibuliwa na wanaoupinga wakimtumia Mwalimu Julius Nyerere kama rejea ya msimamo wao.

Wanakumbushia hotuba yake akiwa Waziri Kiongozi Bungeni, Oktoba  28  1961,  bunge la Tanganyika (sio la Tanzania) kwenye serikali ya madaraka kwamba Mwalimu Nyerere alipinga suala la uraia pacha ambapo alieleza wasiwasi wake kuhusu suala hilo.

 Lakini wale wanaomtumia Mwalimu kama kielelezo cha upinzani wao dhidi ya uraia pacha wanamsoma kwa mtazamo usio sahihi. Wanamwona kama mtu aliyekuwa na msimamo mgumu usiobadilika, wakati ukweli ni kwamba Mwalimu Nyerere hakuwa mtu wa kufikiri kwa namna ya mgando (dogma), bali alikuwa kiongozi aliyekuwa tayari kubadilika kulingana na mazingira, mahitaji ya wakati na changamoto zake.

Kwa kutumia hotuba ya Mwalimu kama hoja ya kupinga uraia pacha, mtu anaweza kuuliza: Je, tunachukulia kila alichosema Mwalimu kama sheria isiyobadilika?

Historia inatuonyesha kuwa Nyerere huyo huyo mara kwa mara alikubali kubadilika na kuachana na sera alizowahi kuzitetea awali, pale alipoona kuwa mahitaji ya wakati yamebadilika.

Mfano wa Azimio la Arusha: Mwalimu Nyerere alisimamia kwa nguvu falsafa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha mwaka 1967. Lakini baada ya miongo kadhaa ya kujaribu sera hii, alitambua kuwa uchumi wa Tanzania unahitaji mabadiliko.

 Nyerere mwenyewe alikubali kuachana na baadhi ya vipengele vya Azimio la Arusha na hatimae alilazimika hata kung’atuka kutoka kwenye nafasi ya urais na kumpisha Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambaye alikuja na sera za uchumi huria.

Kama Mwalimu alikubali kwamba ujamaa ulihitaji maboresho kwa mujibu wa hali halisi, kwa nini basi tumfungie kwenye kauli moja kuhusu uraia pacha wakati dunia imebadilika?

Mfano mwingine ni wa vyama vingi: Mwalimu alikataa mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa miongo mingi, akiamini kuwa chama kimoja kingeleta mshikamano wa kitaifa.

Hata hivyo, alipoona kuwa wakati umebadilika na kwamba Watanzania wanahitaji uhuru wa kisiasa, alikubali mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Huu ni ushahidi mwingine kuwa Nyerere hakuwa na mawazo mgando, bali alikuwa kiongozi aliyefuata mantiki na mabadiliko ya kihistoria.

Kwa hivyo, kumtumia Nyerere kama kisingizio cha kupinga uraia pacha ni kumwelewa vibaya na kuminya fikra zake za kimaendeleo. Ikiwa alikubali mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi na kisiasa kwa kuangalia mahitaji ya wakati, basi tunapaswa kuelewa kuwa hata msimamo wake kuhusu uraia pacha ungeweza kuwa tofauti ikiwa angeishi katika mazingira ya sasa ya utandawazi na harakati za kidiaspora.

ITAENDELEA...

Maoni:  +14374316747

Khaleed_ihaab@yahoo.com