Vyama siasa vilivyo ‘damu damu’ na vyama vya wafanyakazi kila mahali

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 12:20 PM Mar 27 2025
Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere
Picha: Mtandao
Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere

INAPOTAJWA siasa hata kuchimbwa ilikotoka, mbia wake amekuwa vyama vya wafanyakazi. Ikiwekwa nukta mahali hapo, mtu anaweza kujiuliza ni wangapi wanalijua hilo?

Kila inapopekuliwa historia ya siasa ngazi ya dunia, hilo hilo likarudiwa nchini yote yanarejea majibu kwamba pande hizo mbili ni ndugu wa damu.

Mwanzo wa siasa duniani ilikuwa zao la mapinduzi ya viwanda kuanzia ukanda wa Ulaya, mahasusi Uingereza katika miaka ya 1760 hadi kufikia 1840 yalishafikia Marekani.

Kuzaliwa mageuzi hayo nchini Uingereza, kukawapo ukanda wa viwanda katika miji mikubwa iliyokuwa kibiashara kama Derbyshire na Yorkshire.

Jamii ikazaliwa na makundi mawili makuu, moja walio nacho wa viwanda na mashamba makubwa wanakovuna malighafi, kundi la pili la wafanyakazi waaajiriwa wa viwandani, bila kusahau watumwa kutoka mbali.

Pia, huko katika mashamba makubwa ya matajiri wao, ndiko ukawa mwanzo wa malalamiko ya kuonewa katika haki za kazini, malipo kidogo na wanafanyishwa kazi sana.

Kadri vilio hivyo vilizidi na hasa kule kulikoasisiwa mapinduzi viwanda nchini Uingereza, wafanyakazi wakaanza kuunda muungano wakisimama pamoja kudai haki zao katika vikundi hivyo.

Msukumo huo wa wafanyakazi wadai haki ukaunda muungano mkubwa ambao ndio hasa ukawa mwanzo wa kupatikana vyama vya wafanyakazi duniani.

Kila inapotokea dai la kuonewa, wamiliki wa viwandani hadi shambani, wanakumbana na msukumo unaoathiri uzalishaji wao.

Mwisho wa msukumo ukafikia hatua ya kuundwa vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu kamili.

Kadri nyendo zao zilivyosonga, ndivyo ikazaa kuungwa mkono na makundi ya kijamii wanyonge, pia watetezi wa wanyonge.

Kukawapo maisha ya chama cha wafanyakazi Uingereza ikipata kuungwa mkono na watu wenye maisha ya kati, ila watetezi wa wanyonge waitwao ‘Fabian Society’.

Hao wakawasaidia Waingereza wenzao wafanyakazi katika kuongezea nguvu nyendo zao katika ngazi ya kisiasa, hata kukaundwa chama cha Labour. Itikadi yao ikawa kutetea maslahi ya jamii ya watu wa chini, wanaangukia kundi moja na wafanyakazi. 

Wakati katika nchi zinazoendeleza kada ya wanyonge wakionekana zaidi wakulima na wakazi, kwa kuzingatia penye kilimo kunashika sehemu kubwa ya uchumi, wakulima wakiendesha wenyewe, nchi zenye uchumi wa juu, kilimo kinaendeshwa kwa milki ya wawekezaji wakubwa na maana yake watendaji wake wanaangukia kundi la wafanyakazi.

Chama pinzani dhidi ya Labour kiitwacho Conservative, chenyewe kikazaliwa miaka michache baadaye mwanzoni mwa miaka 1900, wanachama wake matajiri wanaowania kuhami maslahi yao kisiasa, ikiwamo vuguvugu la chama chama wafanyakazi wao - Labour.

Ni hadi sasa, vyama vya Labour na Conservative vinabaki kuwa washindani wakuu, utashi na falsafa ikitawaliwa na historia zao.

Labour inasimamia mrengo wa kushoto unaohitaji kulinda maslahi ya wasio nacho kupata ubia na serikali.

Conservative wao wanadumu na mrengo wa kulia wakitaka uhuria zaidi kisera, ili wanufaike na nguvu ya soko kupitia mitaji na miradi ya jumuiya yao.

TANU VS TFL

Katika harakati za siasa nchini, nako kuna wengi wanahoji urafiki wa waliokuwa viongozi wakubwa nchini, Mwalimu Julius Nyerere na Rashid Kawawa.

Mwaka 1954 wakati chama cha TANU kinaanza na nyendo zake chini ya uongozi wa Mwalimu wa Julius Nyerere, huku katika chama cha wafanyakazi ikiwapo Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TFL), chini ya Katibu Mkuu, Rashid Kawawa wakajikuta wanaingia katika ubia.

Nyerere akiwa katika harakati za kutikisa serikali ya ukoloni wa Kiingereza kudai maslahi ya uhuru wa Tanganyika kupitia makundi kama jamii ya kinamama, akavutiwa sana na kinachofanywa na Kawawa huko TFL.

Kawawa alikuwa Katibu Mkuu kijana ambaye moja ya makombora yake, akawezesha mgomo mkubwa wa wafanyakazi nchini kudai maslahi yao.

Ni nafasi ya pekee ikikumbukwa mgomo wa Kampuni ya Bia Dar es Salaam, vilevile kwa wafanyakazi wa Shirika la Reli; huko Tabora. 

Mafanikio ya migomo hiyo ya TFL, ikilazimisha serikali kukaa meza moja, wananchi wafanyakazi kujadili mahitaji yao.

Nikikumbuka mazungumzo yangu naye Mzee Kawawa huko kwake Madale, Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka 2000, akasema harakati zale zilimgusa Nyerere, ambaye akamwalika makao makuu ya TANU, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, wakateta na kuingia ubia wa siri, kuwakabili kwa pamoja watawala wa Kiingereza.

Baada ya hapo akanisimulia kuwa TFL, chini ya Kawawa na TANU wakaendeleza ubia wa siri uliokuwa na mafanikio, hata miaka kadhaa baadaye, Nyerere akavutiwa na kazi yake akimuomba  wajiunge wote TANU.

Kwa mujibu wa aliyonisumulia Mzee Kawawa, baada ya hapo bado hawakukiacha mbali chama cha wafanyakazi, maana hata wadau wake kama Christopher Kassanga Tumbo, aliyeongoza mgomo wa reli Tabora, akajitokeza katika siasa wakishirikiana hata baada ya uhuru.

Tumbo hata baadaye ndiye akawa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Uingereza, kabla ya kuingia katika msuguano na serikali, akirejea nyumbani.

CHAMA KIMOJA

Tanganyika, ikiingia katika Muungano mwaka 1964, itikadi rasmi ya kijamaa na mfumo wa chama kimoja, iliibeba Chama cha Wafanyakazi kilichokuwa sehemu ya jumuiya ya TANU, sambamba na vijana, pia wanawake.

Kuanzishwa Jumuiya ya Wafanyakazi (NUTA) ikazawadiwa na nyenzo ya kijamiii ambayo wakati huo ilikuwa na mvuto mkubwa kijamii, bendi ya muziki ya NUTA, ambayo imepitia mabadiliko mengi, sasa iko huru kwa jina la Msondo Ngoma.

Ilikuwa sehemu ya kurejesha shukurani kwa kada ya wafanyakazi na wadai wake wengine, kufaidi matunda ya uhuru,

Kuhitimisha mfumo wa kijamaa na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa mwaka 1964 hadi 1969, ilitangaza kutaifisha mashirika, mifumo ya uzalishaji na uwekezaji kitaifa mwaka 1967, kupitia Azimio la Arusha.

Hiyo ikaendana na uwekezaji mkubwa kitaifa ikiwamo katika huduma na mahitaji ya msingi, viwanda kama vya nguo, shule na zahanati.

Ni zama ambazo serikali ikapata uwekezaji mkubwa kutoka marafiki mataifa kama China, Kiwanda cha Nguo Urafiki, unaodumu hadi sasa, viwanda kama cha nguo Urafiki, lilipoanzishwa.

SCOPO NA BARAZA KUU

Zao lake kukawapo mlipuko mkubwa  wa mashirika ya umma na wafanyakazi wake. Serikali hadi inahitimishna hatua ya kwanza ya mpango wake wa maendeleo, mwaka 1969, serikali ikarejeshea shukurani tena za kisiasa kwa kundi hilo la wafanyakazi, ikibuni mambo makuu mawili.

Kuna sheria iliyobuniwa mwaka 1969, ikiwezesha kuundwa Tume ya Rais ya Kusimamia Mashirika ya Umma (SCOPO), ambako kunapatikana kundi kubwa la wafanyakazi.

Ni sheria iliyopata hata kurejewa kwa kigezo cha kutafsiri kiwango cha mtumishi wa umma, kuanzia, cheo hadi maslahi.

Pia, katika sheria hiyo ikazama kuanisha tafsiri ya Mashirika ya Umma, kuwa chombo au taasisi yoyote inayomilikiwa na serikali kwa zaidi ya asilimia 51, huku msamiati SCOPO ikajulikana kwa kila mfanyakazi kama mizania ya maisha yake.

Vilevile kukaundwa chombo hicho, kilichohudumu chini ya Ofisi ya Rais, ikiwa  ishara wazi kuw Rais Julius Nyerere wakati huo, aliipa uzito mkubwa.

Hata hivyo, sheria hiyo imeshafanyiwa maboresho mwaka 1992 ikitaja shirika la umma sasa ni mahsusi kwa inayohusika na uzalishaji au kibiashara.

Kukazaliwa zawadi nyingine wakati huo, TANU ikishika hatamu kupitia Mkutano Mkuu wa TANU mwaka 1970, ukaagiza kuundwa kwa Baraza Kuu la Wafanyakazi kila sehemu yanayokutana kila mwaka kutatua ketio na maendeleo yao kazini. Kwa sasa imo katika Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004, ikiwa sehemu ya kutetea haki ya mtumishi.

KUBUNIWA CSR

Hatua zaidi za wakati wa utekelezaji Mpango wa Pili wa Maendeleo 1969 – 1974 ukawa na maudhui ya kurejesha shukurani kwa wafanyakazi, yalifanikshwa katika mapinduzi viwanda na taasisi za msingi awamu ya kwanza na yakawa yanaendelezwa.

Hapo kukabuniwa kinachoitwa Uwajibikaji wa Taasisi kwa Jamii (CSR), ambacho kinaonekana. Ingawa kililenga Watanzania wote, njia yake kuu ilipitishwa katika taasisi na idara za umma.

Ni wakati huo huduma takriban zote zilitolewa bure, ikiwamo elimu na tiba, hivyo CSR ya wakati huo ilirejea penye utashi uchi wa umma ulikozama; michezo na burudani.

Muziki wa dansi ukiwa katika upeo wake, hata soko la Tanzania kuvutia wanamuziki wengi, nayo mashirika ya umma yakaelekezwa kuanzisha nguzo burudani na michezo, ikiwa sehemu ya CSR.

Unapoziona bendi za muziki kama Bima Lee Orchestre, DDC Mlimani Park- Sikinde, Uhamiaji Jazz wana ‘Hamaha’ Polisi Jazz ‘Vangananga’ta, JKT Kimbunga na JKT Mafinga’ Kimulimuli;, Mwenge Jazz Band ‘paselepa’, Magerzea Jazz, zote zilikuwa njia ya wananchi kurejeshewa shukurani, kwa nguzo ya mtumishi nao wakifikishia umma CSR .

Kumea bendi hizo zilidiriki kuzamisha bendi binafsi maarufu zilizokuwapo, kutokana na msukumo wake wa ajira na kufanya bendi kama vile Safari Tippers, Western Jazz ‘saboso’ na Tabora Jazz na Dar Jazz kutoweka.

Hadi kufika mwaka 1978, CSR ya muziki ilikuwa juu kitaifa, hata mwaka 1979 Mzaire King Kikuu akitunga kusifu “Dar es Salaam” yachemka kama bahari” kwa burudani (ya CSR) kila mahali.

Hata katika katika michezo kukazalishwa timu kama Usalama inayounganisha idara za usalama, viwandani; Viatu Bora waliong’ara katika ligi ya Wilaya Temeke hadi mkoa Dar es Salaam, majirani zao Sigara, na Ndovu ya Arusha.

Vivyo hivyo, ikawa siri ya kuma mpira wa netiboli hadi kukiwa na timu kama Jeshi Stars, Bima na Bora zilizovuma na nyota zao kina Amina, Asha Baraka na Judith Chifupa wakitikisa viwanja kama Reli Gerezani, Dar es Salaam, Tanzania kuna wakati ikachukua ubingwa wa Afrika Mashariki.

Hiyo ndio ikawa vilevile kwa mpira wa vikapu uking’ara na timu kama za Benki Kuu, huku riadha kunapatikana vinara wa kimataifa kama Mwinga Mwanjala, Filbert Bayi bingwa wa dunia mita 1,500, hali kadhalika kwa Juma Ikangaa. Yote hayo ni kazi ya CSR kupitia sehemu za kazi.