MWEKEZAJI kutoka Tanzania, Edhah Abdallah Munif, anaweza kukwama katika mpango wake wa kununua asilimia 29.2 ya hisa za Kampuni ya East African Portland Cement (EAPC) kutoka kwa kampuni ya Uswisi ya Holcim, kufuatia hatua ya Bunge la Kenya kuingilia kati mchakato huo kwa madai ya bei kuwa ya chini mno na kulinda maslahi ya taifa.
Katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Ushirika, wabunge walipinga uuzaji huo wakidai kuwa hisa hizo zinauzwa kwa nusu ya thamani ya soko, na kuonya kuwa kampuni ya Munif – Kalahari Cement – huenda inalenga zaidi ardhi yenye thamani ya zaidi ya Ksh bilioni 20 kuliko uendeshaji biashara ya saruji.
Kamati hiyo sasa inapendekeza EAPC inunue hisa hizo yenyewe (share buyback) kwa bei ya soko, badala ya kuuziwa kampuni ya nje kwa bei ya Ksh 27.30 kwa hisa, wakati hisa hizo zilikuwa zikifanya biashara kwa Ksh 56 katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).
"Kwa nini mnasubiri hisa ziuzwe kwa watu wa nje? Kwa nini msizinunue ninyi wenyewe kwa manufaa ya Wakenya?" alihoji Mbunge wa Kajiado Kusini, Samuel Parashina. Endapo EAPC itatekeleza mpango huu, itakuwa kampuni ya tatu nchini Kenya kufanya 'share buyback' baada ya Nation Media Group (2021) na Centum (2023).
Hii ni mara ya pili kwa Munif kukumbwa na mvutano nchini Kenya katika harakati zake za kutanua ushawishi katika sekta ya saruji. Miezi michache iliyopita, kampuni yake nyingine ya Amsons Group ilinunua Bamburi Cement kwa Ksh bilioni 23.6 – ununuzi uliomfanya kuwa mwekezaji mkubwa zaidi wa saruji nchini Kenya.
Kwa kuwa Bamburi Cement inamiliki asilimia 12.5 ya EAPC, ununuzi wa asilimia 29.2 kutoka Holcim ungemfanya Munif kumiliki jumla ya asilimia 41.7, hivyo kuwa mwanahisa mkuu wa EAPC.
Hisa zinazouzwa ni milioni 26.32. Bei ya makubaliano ni Ksh 27.30 kwa hisa na thamani ya mkataba ni Sh. milioni 718.7.
Thamani ya soko (NSE) ni Ksh 56 kwa hisa, thamani ya soko ya kampuni ni Ksh bilioni 5.55, thamani ya vitabu ya EAPC ni Ksh bilioni 20.4, mali zote za kampuni ni Ksh bilioni 35.19 na madeni ya kampuni ni Ksh bilioni 14.79.
Wabunge walisisitiza kuwa makubaliano hayo yanaipa Kalahari Cement fursa ya kununua kwa bei ya kutupa mali ya thamani kubwa, huku masharti ya mkataba huo yakiwa hayajafichuliwa kikamilifu kwa umma.EAPC inamiliki ekari 4,626 za ardhi – sehemu kubwa ikiwa chini ya mikataba ya upangishaji wa muda mrefu, na thamani yake inakadiriwa kuwa Ksh bilioni 21.23.
Wabunge wameeleza wasiwasi kuwa Kalahari Cement inaweza kununua kampuni kwa bei ya chini, kisha kuuza ardhi hiyo kwa faida kubwa, na hivyo kuathiri ustawi wa kampuni na uchumi wa ndani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA), Wyckliffe Shamiah, alisema CMA haina mamlaka ya kuamuru bei ya hisa, kwa kuwa hiyo ni makubaliano kati ya muuzaji na mnunuzi.
Hata hivyo, ameahidi kuchunguza iwapo mchakato huo unafuata kanuni na kama unalinda maslahi ya umma. Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji wa EAPC, Mohammed Osman, alisema kampuni ina uwezo wa kufanya ‘share buyback’ kama Bunge litatoa maelekezo rasmi.
"Tumeanza kufufua kampuni na tuna mtiririko mzuri wa fedha. Tunaweza kulipa kiasi hicho kwa kutumia faida yetu," alisema Osman.Mpango huu unaweza kuwa jaribio la nia ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuruhusu uwekezaji wa kuvuka mipaka. Ikiwa Kenya itaweka vizingiti kwa mwekezaji kutoka Tanzania, licha ya mkataba wake halali na Holcim, inaweza kuzua maswali kuhusu uwazi na usawa katika masoko ya pamoja ya kanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED