Mgombea Urais Colombia apigwa risasi

By News Agency , Agency
Published at 02:33 PM Jun 08 2025
Miguel Uribe Turbay, seneta mwenye umri wa miaka 39 na Mgombea Urais Colombia alishambuliwa alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake
PICHA: MTANDAO
Miguel Uribe Turbay, seneta mwenye umri wa miaka 39 na Mgombea Urais Colombia alishambuliwa alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake

Mgombea urais wa Colombia yuko katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi tatu ikiripotiwa mara mbili kichwani katika hafla ya kampeni katika mji mkuu, Bogota.

Miguel Uribe Turbay, seneta mwenye umri wa miaka 39, alishambuliwa alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake kwenye bustani siku ya Jumamosi. Polisi walimkamata mshukiwa mwenye umri wa miaka 15 katika eneo la tukio, ofisi ya mwanasheria mkuu ilisema.

Mkewe Uribe, Maria Claudia Tarazona, alitoa wito kwa taifa kumuombea aokoke. “Miguel kwa sasa anapigania maisha yake, tumuombe Mungu aongoze mikono ya madaktari wanaomhudumia,” alisema. Chama cha Uribe Centro Democratico kimelaani shambulio hilo, na kulitaja kuwa tishio kwa "demokrasia na uhuru nchini Colombia".Picha za simu zilizosambazwa mtandaoni zinaonekana kuonyesha wakati alipopigwa risasi kichwani katikati ya hotuba, na kuwafanya waliokusanyika kukimbia kwa hofu.

Wahudumu wa afya walisema alipigwa risasi kwenye goti na mara mbili kichwani, shirika la habari la AFP liliripoti. Alisafirishwa kwa ndege hadi hospitali ambapo wafuasi walikusanyika kufanya mkesha. Uribe alifanyiwa upasuaji na alikuwa katika saa za kwanza muhimu za kupona, Meya wa Bogotá Carlos Fernando Galán alisema Jumamosi usiku.