Rais wa Marekani Donald Trump amesema uhusiano wake na Elon Musk umekwisha.

By News Agency , Agency
Published at 02:32 PM Jun 08 2025
Rais wa Marekani Donald Trump
PICHA: MTANDAO
Rais wa Marekani Donald Trump

"Ninadhani hivyo," Trump aliiambia NBC News Jumamosi, alipoulizwa ikiwa alifikiri uhusiano wa karibu wa wawili hao umekwisha. Alijibu "Hapana" alipoulizwa kama alitaka kurekebisha mahusiano yaliyoharibika.

Maoni hayo yalikuwa ya hivi karibuni zaidi ya Trump tangu mzozo mkubwa kati yake na Musk kuzuka kwenye mitandao ya kijamii. Hatua hiyo imekuja baada ya bilionea huyo wa teknolojia, ambaye alitoa mamilioni kwa kampeni ya uchaguzi wa Trump na kuwa msaidizi wa White House, kukosoa hadharani muswada wa ushuru na matumizi wa rais, sera muhimu ya ndani.

Kwa wiki kadhaa, Musk amekuwa akiikosoa muswada huo uliopewa jina la "Big Beautiful Bill", ulipokuwa ukipitia Congress. Alisema muswada huo ukipitishwa utaongeza matrilioni ya dola kwenye nakisi ya kitaifa na “kudhoofisha” kazi aliyoifanya akiwa mkuu wa Doge, Idara ya Ufanisi wa Serikali na juhudi zake za kubana matumizi ya serikali.

Muda mfupi baada ya kuachana na Doge baada ya siku 129 kazini, Musk alichapisha kwenye tovuti yake ya kijamii ya X kwamba muswada huo ulikuwa "chukizo", lakini hakumkosoa Trump moja kwa moja.

Siku ya Alhamisi, hata hivyo, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa "amesikitishwa" na tabia ya Musk. Musk alijibu kwa msururu wa machapisho kwenye X, akisema kwamba Trump angepoteza uchaguzi bila yeye na kumshutumu Trump kwa kuhusishwa na faili za Jeffrey Epstein, mfadhili aliyefedheheshwa ambaye alikufa gerezani akisubiri mashtaka ya biashara ya ngono.

Trump alijibu kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akisema kwamba Musk alikuwa "wazimu". Katika chapisho moja, alitishia kukata kandarasi za Musk na serikali ya shirikisho. Katika mahojiano yake na NBC News siku ya Jumamosi, Trump alisema Musk amekuwa "akikosa heshima kwa ofisi ya rais".


Chanzo: BBC