MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameipongeza shule ya sekondari Don Bosco, iliyopo Didia wilayani Shinyanga, kwa kuendeleza utamaduni wa michezo shuleni, kwamba inasaidia kuibua, kukuza vipaji vya wanafunzi na kuimarisha afya zao.
Mtatiro amebainisha hayo, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika uhitimishaji wa wiki ya michezo ya Don Bosco, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mtatiro amesema michezo kwa wanafunzi ni muhimu kwa kuimarisha afya zao, kuibua vipaji, kuwajengea nidhamu, kupumzisha akili na hata kufanya vizuri kitaaluma.
Ameongeza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya maisha ya kila mtu na wataalamu wa afya wanasisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi, ili kuepukana na magonjwa nyemelezi.
Pia, ametoa nasaha kwa wanafunzi, akiwashauri waendelee kushiriki michezo kuwa na nidhamu na kupenda masomo, ili waweze kutimiza ndoto zao na kuwa viongozi bora wa baadaye katika taifa hili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Don Bosco, Padri Amani Meela, amesema kuwa shule hiyo inatambua umuhimu wa michezo na kwamba michezo shuleni hapo, ni sehemu ya malezi ya watoto na inajenga nidhamu, kukuza ufanisi wa kitaaluma, kuboresha afya na kuibua vipaji.
Kaka Mkuu wa shule hiyo, Meshack Hunge, amesema michezo hiyo kwao inawajenga kiafya, kiakili, kuibua vipaji vyao, kuimarisha udugu, sababu katika michezo hiyo huwa wanaalika shule za jirani kushiriki na kufurahi pamoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED