Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuwa kuanzia kesho, Jumamosi Aprili 5, 2025, baadhi ya noti za zamani hazitatambulika tena kama fedha halali. Zoezi la kuziondoa noti hizo lilianza Januari 6, 2025, na linakamilika rasmi kesho.
Noti zitakazositishwa ni zile za Sh20, Sh200, Sh500, Sh1,000, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 zilizotolewa kati ya mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya Sh500 ya mwaka 2010.
BoT imeeleza kuwa baada ya tarehe hiyo, hakutakuwa na malipo yoyote yatakayofanywa kwa noti hizo, wala benki kuruhusiwa kupokea au kubadilisha fedha hizo.
Tangazo hilo limetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, sura ya 197 kifungu cha 28 (2) na (3), inayotoa mamlaka kwa BoT kusitisha uhalali wa noti kwa kuchapisha tangazo kwenye Gazeti la Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu wa BoT, Ilulu Ilulu, amesema zoezi hilo ni la kawaida na wananchi walipewa muda wa miezi mitatu kubadilisha noti hizo kwa thamani ile ile kabla ya muda wa mwisho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED