Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kwa mwezi Aprili, zitakazotumika kuanzia leo.
Kwa mwezi huu, gharama za uagizaji mafuta (premiums) zimepungua kwa wastani wa asilimia 6.08 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.09 kwa mafuta dizeli na kuongezeka kwa asilimia 1.11 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam, huku bandari ya Tanga kukiwa hakuna mabadiliko, na kwa bandari ya Mtwara zimepungua kwa wastani wa asilimia 4.00 kwa mafuta ya petroli na dizeli.
Katika bei kikomo kwa mwezi Aprili 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.92 ya kwa mafuta ya petroli, asilimia 6.57 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 7.82 kwa mafuta ya taa mtawalia. Bei zinazozingatiwa za mafuta yaliyosafishwa (FOB) ni za soko la Uarabuni.
Kwa bei za mwezi Aprili 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umeongezeka kwa asilimia 1.91, huku EWURA ikiwataka wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na atakayekiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED