JESHI la Magereza limeingia makubaliano ya kutumia mbolea zinazozalishwa na kiwanda cha Itracom Fertilizer LTD kilichoko jijini hapa, ili kuboresha shughuli za kilimo ikiwamo kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu, alisema hayo juzi wakati wa maonesho ya ufanisi wa mbolea za FOMI zinazotengenezwa na kiwanda hicho, katika shamba darasa la jeshi hilo lililoko makao makuu, Msalato jijini hapa.
Kamishna Jenerali Katungu aliushukuru uongozi wa kiwanda hicho kwa kuona umuhimu wa kujenga ushirikiano baina yao ambao anaamini utazidi kukuza sekta ya kilimo ndani ya jeshi hilo, ikiwamo kuongeza uzalishaji kutokana na kulima kitaalamu kwa kutumia mbolea stahiki katika mazao ya chakula na biashara.
"Tunawashukuru sana Itracom Fertilizer kwa kukubali kushirikiana nao katika kuendesha shughuli za kilimo naamini tutafika mbali kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara," alisema Katungu.
Aidha, alisema jeshi hilo litaendeleza ushirikiano na Intracom ili kuzalisha kwa tija ikiwa ni maelekezo ya serikali kuwa Jeshi la Magereza kuongeza uzalishaji ili kujitosheleza kwa chakula.
Kamishna Jenerali Katungu alitoa rai kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kutembelea shamba darasa la Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujifunza mbinu bora za kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kuingia makubaliano ya ushirikiano na kiwanda hiko ili kuboresha shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara jeshini.
Senyamule alisema kutokana na umahiri lilio nao Jeshi la Magereza kwenye sekta ya kilimo, anaamini ushirikiano wao baina ya kiwanda cha uzalishaji mbolea cha Itracom utazidi kuongeza uzalishaji katika mazao mbalimbali wanayolima.
Mkuu wa Mkoa alisema shamba darasa la Jeshi la Magereza ni mfano bora wa kuigwa, huku akiwataka wakulima mbalimbali kujitokeza kujifunza shughuli za kilimo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED