Waendeshaji Bahati Nasibu ya Taifa wazidi kujiimarisha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:14 PM Apr 03 2025
Mkurugenzi wa ITHUBA nchini, Kelvin Koka
PICHA: MTANDAO
Mkurugenzi wa ITHUBA nchini, Kelvin Koka

KAMPUNI ya ITHUBA iliyopewa jukumu na serikali kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa, imeendelea kujiimarisha kuhakikisha inawafikia watanzania wengi ili kuboresha maisha yao na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano na mmoja wa watoahuduma za malipo kwa njia ya simu nchini jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa ITHUBA nchini, Kelvin Koka alisema ushirikiano na mtoahuduma huyo umelenga kuwafikia mamilioni ya wananchi.

"Ili kuhakikisha watanzania wanashiriki katika michezo ya bahati nasibu kwa urahisi mara tu Bahati Nasibu ya Taifa itakapozinduliwa rasmi, ushirikiano huu utarahisisha upatikanaji, ununuzi na ulipaji tiketi kwa urahisi na usalama," alisema Koka

Alisema wachezaji wa bahati nasibu hiyo watashiriki kwa kutumia mbinu madhubuti za malipo kwa kutumia mtoahuduma huyo kuhamisha miamala kutoka benki, mawakala wa mtoahuduma ambao ni zaidi ya 30,000 nchi nzima.

Alisema wachezaji wataweza kununua tiketi na kupokea malipo ya ushindi kupitia majukwaa ya fedha kwa njia ya simu, vituo vya malipo na miamala ya kidijitali.

"Hii ni hatua kubwa katika sekta ya michezo ya kubahatisha nchini, kwa kushirikiana na mtoahuduma katika huduma za kifedha ili kila mtanzania bila kujali mahali alipo nchini, ashiriki kikamilifu katika michezo hii ya kusisimua ya bahati nasibu," alisema.

Alisema bahati nasibu hiyo mbali na kuburudisha, inalenga kuleta maendeleo kwa wananchi. Sehemu ya mapato yatokanayo na mauzo ya tiketi za bahati nasibu yatatengwa kwa ajili ya miradi muhimu kama vile kuendeleza vipaji vya vijana chipukizi na sekta nyingine zinazogusa jamii.