Akamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mkewe Kibaha

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:53 PM Dec 04 2024
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Godfrey Killu (30), mkazi wa Mbwate, Kata ya Mkuza, Wilaya ya Kibaha, kwa tuhuma za mauaji ya mke wake Elizabeth Sindikila (26).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema tukio hilo lilitokea Desemba 1, baada ya wawili hao kwenda kunywa pombe za kienyeji. Walipokuwa wakirudi nyumbani, walizozana baada ya Elizabeth kugoma kuondoka, hali iliyopelekea ugomvi kati yao.

"Godfrey alitumia fimbo kumpiga Elizabeth sehemu mbalimbali za mwili ili kumlazimisha kwenda nyumbani. Baadaye alipoona hali ya mke wake si nzuri, alimkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu, lakini alifariki akiwa anapatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata," alisema Kamanda Morcase.

Kamanda huyo ameongeza kuwa mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo wakati wa mahojiano. Tayari upelelezi unaendelea, na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.