Rollers skate kunogesha kampeni utalii wa ndani Ngorongoro

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:57 PM Dec 04 2024
Meneja Idara ya utalii na Masoko wa NCAA, Kamishna Mwandamizi Msaidizi, Mariam Kobelo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Meneja Idara ya utalii na Masoko wa NCAA, Kamishna Mwandamizi Msaidizi, Mariam Kobelo.

MAMLAKA ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanza kuwatumia vijana maarufu wa Arusha, wanaofanya mchezo wa kuteleza na viatu vya matairi ‘Rollers Skate’ kuvutia watalii wa ndani nchini, kutembelea vivutio vyake.

Wakati Ngorongoro ikija na ubunifu huo, inaelezwa kwamba idadi ya watalii wa ndani wanaotembelea eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imeongezeka kati ya Julai na Novemba mwaka huu baada ya kufikiwa na watu 200,000.

Akitangaza leo, Disemba 4 mwaka huu Jijini Arusha, kuanza rasmi kwa kampeni maalum ya kuchochea ongezeko la watalii wa ndani, maarufu kama Merry & Wild, Ngorongoro Awaits, Meneja Idara ya utalii na Masoko wa NCAA, Kamishna Mwandamizi Msaidizi, Mariam Kobelo, amesema kampeni hiyo itawawezesha Watanzania wengi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro.

Kampeni hiyo iliyoanza Disemba 4 itafikia ukomo wake Januari 4 mwaka 2025.

“Mamlaka ya Ngorongoro tumeamua kuanzisha kampeni hii kwa mwaka huu ili kuwawezesha Watanzania wengi kutembelea maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro ili kujionea na kushuhudia uzuri wa vivutio vilivyopo.

“Takwimu zinaonyesha watalii wa ndani wanaotembelea vivutio vya utalii imezidi kuongezeka kuanzia Julai hadi Novemba 2024 wamefikia 2024.”

Vijana wa Arusha wanaocheza mchezo wa kuteleza na viatu vya matairi wakinogesha Kampeni za Merry & Wild, Ngorongoro Awaits.

Ameyataja maeneo yenye vivutio ni kama urithi wa utamaduni wa Olduvai, Kreta ya Empakai, Olmoti na Mlima wa tatu kwa urefu Tanzania wa Loromalasi. 

“Watanzania watakaoitembelea Ngorongoro watanufaika na vivutio vya msimu wa Ndutu, kwa kujionea idadi kubwa ya nyumbu waliorejea nchini kwa ajili ya kujifungua, kabla hawajahama tena kwenda Hifadhi ya Masai-Mara, nchini Kenya.

Pia, yapo Makumbusho ya Jiolojia ya Ngorongoro maarufu kama Ngorongoro- Lengai UNESCO Geopark.

Akizindua kampeni hiyo, Katibu Tawala Msaidizi, Mkoa wa Arusha, anayeshughulikia uchumi na uzalishaji mali, Daniel Loiruck, amesema mpango wa kuboresha sekta ya utalii Mkoa wa Arusha upo mbioni.

Alisema Mkoa huo, unaunga mkono kampeni hiyo ya kuhamasisha watanzania kupenda kutembelea vivutio vya utalii katika hifadhi mbalimbali chini.