RAIS wa Marekani, anayemaliza muda wake, Joseph Biden, ameanza mwezi Desemba 2024 kwa kuitembelea Afrika.
Ni ziara inayomfikisha Angola taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta Kusini ya Jangwa Sahara, kufanikisha uwekezaji wa miundombinu ya reli itakayofanikisha kupata madini muhimu yanayohitajika duniani leo.
Safari ya Biden inalenga kushughulikia uwekezaji katika Ukanda au ‘Corridor’ ya Lobito, mradi wa reli ya maili 800 sawa na kilometa 1,600 unaounganisha Congo na Angola kusafirisha madini kutoka Congo kwenda Marekani na Ulaya, inasema televisheni ya Marekani ya CNN.
Ni uwekezaji unaoungwa mkono na Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) ukilenga kusafirisha madini muhimu kutoka Afrika hadi bandari ya magharibi ya Angola ya Lobito kwa ajili ya kuyafikisha nchi za Magharibi, kwa mujibu wa CNN.
Mpango huo ni kitovu cha juhudi za utawala wa Biden za kuongeza uwekezaji barani Afrika ili kuipunguzia kasi China kuwa na nguvu Afrika.
Inakumbusha kuwa China imemwaga mabilioni ya dola katika miradi ya miundombinu bara zima katika muongo mmoja uliopita.
Septemba mwaka huu, Rais wa China Xi Jinping wa China aliahidi msaada wa dola bilioni 50 kwa bara hilo na pia msaada wa masuala ya kijeshi.
Rais Biden pia atatembelea visiwa vya Cape Verde, akikutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Ulisses Correia Silva.
Rais Biden anazuru bandari ya Lobito na kutembelea kiwanda cha kusindika chakula cha Carrinho, televisheni hiyo inaongeza.
Ukanda wa Lobito ni wa kwanza wa kimkakati wa kiuchumi unaosisiwa na Ushirikiano wa mataifa tajiri zaidi duniani G7 wa miundombinu na uwekezaji wa kimataifa (PGII) Mei 2023.
Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) zimeamua kuwekeza kwenye ukanda huo utakaofanikisha kuchimba madini hayo kutoka Congo na kuyapeleka kwenye viwanda vyao.
Mataifa yanayopitiwa na reli hiyo ni Angola, Congo DRC na Zambia pamoja na Tanzania kwa kuwa inatarajiwa kuendelea hadi kuwa na tawi kwenye Bahari ya Hindi.
ANAIMALIZA AFRIKA
Msomi na mchambuzi wa masuala ya maendeleo , ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUTI Mwanza, Dk. Kamugisha Byabato, anapinga usafirishaji madini hayo.
“Waangola na Waafrika wanapokubali mradi huo ni aibu hawajisaidii wala Afrika. Kinachofanyika ni mwendelezo wa siasa za ukoloni mkongwe ulioanza miaka 1880 kwenye mkutano wa kuigawa Afrika.”
“Kwanini msimamo usiwe Marekani na EU kuwekeza viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazotokana na madini hayo ya kimkakati? Bidhaa ni kama betrii za magari yanayotumia umeme, vifaa vya simu, ndege na bidhaa zote za kielektroniki?” anahoji Dk. Byabato.
Anashauri kijengwe kiwanda Angola au DRC na siyo kuchukua mali ghafi za Afrika leo baada ya miaka 150 ya mgawanyo wa Afrika uliofanyika Berlin Ujerumani.
“Afrika iamke sasa kuendeleza miundombinu ili koboresha unyonyaji siyo suala jema. Kwa mfano Wajerumani walivyochukua makoloni Afrika, walipanga kujenga reli kutoka Namibia hadi Tanganyika kuunganisha himaya zao.
Tukumbuke baada ya kuigawa Afrika eneo lililo katikati ya Bahari ya Hindi na ya Atlantic liliitwa Congo Free Trade Area, ili kuruhusu liwe wazi kwa yeyote anayetaka kuvuna raslimali achukue .” anakumbusha mhadhiri huyo.
Anafurahia kujengwa reli hiyo na nyingine nyingi za kuunganisha nchi za Afrika, miji na miji na kanda kwa kanda kama ilivyo TAZARA akikumbusha kuwa ipo reli ya Trans Siberian Railways inayounganisha Ulaya Mashariki na Magharibi ikipita chini ya bahari hadi Urusi kwenye mji wa Vladivostok ambayo pia ni jirani na Japan.
Anaongeza kuwa kujenga reli ya Lobito DRC, Zambia hadi Tanzania ni jambo la kimkakati na bora zaidi kwa kuboresha mawasiliano kusini mwa Sahara na zinahitajika reli nyingi zaidi “Itoke Dar es Salaam hadi Conacry Guinea, Cairo hadi Cape Town. Pamoja na barabara za kisasa na kuwepo mabasi ya kuzunguka miji mikuu ya Afrika nzima na si tena miundombinu ya kusafirisha raslimali za Afrika na kuiachia umaskini.” Anaonya Byabato.
Kama zinavyoundwa ndege kuna kampuni zinatengeneza mabawa, injini, vipuri, vioo, mifumo ya umeme, ulinzi na umbo.
Lakini ni katika nchi mbalimbali pale kampuni husika ya kutengeneza ndege zinanunua vipuri na kuunganisha ili kupata ndege kamili, anaeleza.
Kuchukua kila kitu kutoka Afrika huku mataifa yakifurahia kana kwamba ni mafanikio wakati hatua hiyo ni sawa na ukoloni mkongwe na utandawazi unaoendeleza ubeberu, ni jambo la kukataa, anaongeza..
TRUMP ATAKUBALI?
Anapoulizwa iwapo mradi huo utafanikiwa kwa sababu Biden, anaondoka na Rais Donald Trump anachukua uongozi anajibu.
“Marekani ina sera ya mikakati ya kitaifa na kiongzi anayeingia ikulu haibatilishi. Kwa mfano wanasimamia na kulinda masuala makubwa ya kitaifa kama ulinzi, usalama, uwekzaji na biashara, kwa hiyo hata kama Rais Biden anaondoka mwezi ujao na Trump anachukua uongozi kama ni suala la kitaifa litaendelea.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED