Aokotwa mtaani amefariki dunia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:55 AM Dec 29 2024
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)  Pius Lutumo
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Pius Lutumo

MWANAMKE mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30 amekutwa akiwa amefariki dunia katika eneo la Mtaa wa Mtakuja Kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)  Pius Lutumo, alisema mwili wa marehemu huyo uliokotwa ukiwa hauna jeraha  Desemba 28, majira ya saa 10:00 asubuhi katika eneo lenye uwazi mtaani hapo.

“Hadi sasa waliofika eneo la tukio hawakuweza kumtambua marehemu huyo na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma," alisema.

 Kamanda Lutumo alisema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi juu ya kifo cha mwanamke huyo ili kubaini utambulisho wake sambamba na chanzo cha kifo chake.

Kamanda Lutumo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mara kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kabla ya matukio hayajatokea, ili wahusika waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za hapa nchini.