ASKOFU wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Michael Hafidh, amenusurika katika ajali mbaya iliyotokea juzi Handeni, Tanga ikihusisha basi la abiria na lori na kuua watu 11 na wengine 13 kujeruhiwa.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:00 usiku baada ya lori aina ya Mistubishi Fuso lililokuwa likitolea Lushoto kwenda Dar es Salaam kugongana na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Mkata, wilayani handeni, kwenda jijini Tanga.
Mmoja kati ya viongozi wa juu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Makao makuu Dodoma, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alithibitisha Askofu Hafidh kupata ajali hiyo kisha kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu na sasa anaendelea vizuri.
Juzi, Umoja wa Anglikana wa Kueneza Injili kupitia mtandao wa kijamii wa ‘facebook’ ulieleza kuwa Askofu Hafidh alipata ajali akiwa katika basi la abiria liligongana na lori na kujeruhiwa kisha kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na majeruhi wengine.
Taarifa hiyo ilisema kutokana na hali hiyo Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes, na viongozi wengine wa dini walikwenda kumtembelea na kumjulia hali.
Aidha, taarifa hiyo ilisema Askofu Hafidh alipotembelewa na viongozi hao, alimtambua Askofu Sosthenes, hali iliyoonesha kuwa kuna unafuu wa afya yake tofauti na alipokuwa amefikishwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili lilizipata na kuthibitishwa na Ofisa Uhusiano kwa Umma wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Abdallah Nassoro, zilieleza kuwa Askofu Hafidh, anaendelea na matibabu katika taasisi hiyo baada ya kuhamishiwa kutoka MNH.
“Ni kweli Askofu yupo hapa MOI anaendelea na matibabu baada ya kuhamishiwa kutokea Muhimbili. Ninachoweza kusema ni kwamba yuko hapa anaendelea na matibabu,” alisema Nassoro.
ASKOFU MWAMAKULA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula, katika ukurasa wake wa facebook, alieleza kusikitishwa na taarifa hiyo na na kuliomba Kanisa la Tanzania kumuombea Askofu Hafidh pamoja na majeruhi wote ili Mungu awafanyie wepesi na kuwaponya.
Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Handeni , Wakili Albert Msando, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa majeruhi 13 walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kupata matibabu.
“Watu 11 walifariki dunia wakiwamo madereva wa magari yote mawili na majeruhi 13 wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kupata matibabu. Kati yao majeruhi tisa hali zao si nzuri na madaktari wanaendelea na juhudi za matibabu,.
“Tuendelee kuwaombea familia za watu wote waliofariki katika ajali hiyo. Mungu akawakumbuke marehemu waliofariki. Raha ya milele uwape, Ee Bwana. Mwanga wa milele uwaangazie. Wapumzike kwa amani,” alisema.
KAULI ASKOFU MKUU
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo Mndolwa, aliwaeleza waumini wa kanisa hilo kuwa hali ya afya ya Askofu Hafidh, inaendelea kuimarika.
Askofu Dk. Mndolwa alitoa kauli hiyo jana kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Shukrani ya Familia ya Askofu Mkuu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Patrick Bagamoyo, Dinari ya Vugiri, Korogwe.
Alisema Askofu Hafidh alikuwa miongoni mwa wasafiri waliopata ajali ya gari iliyotokea mapema juzi katika eneo la Kwenkwale, kata ya Kitumbi, Handeni mkoani Tanga.
“Tumepokea taarifa za ajali ambayo imesababisha vifo vya baadhi ya wasafiri na majeruhi akiwamo Askofu Hafidh ambaye licha ya majeraha aliyoyapata, tunamshukuru Mungu alitoka salama na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema
Askofu Dk. Mndolwa alisema kanisa linatoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo na kuwaombea majeruhi wapone haraka ili warudi kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED