ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula, ametoa ujumbe mzito akiitaka serikali kushughulikia changamoto sita zinazoikabili jamii ili washerehekee sikukuu ya Krismasi wakiwa na amani mioyoni mwao.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni usalama wa maisha ya watu na mali zao, ukosefu wa ajira, uhalifu wa kisiasa, gharama za maisha, gharama za matibabu na ubora wa elimu.
Alisema mambo hayo yanabeba msingi wa haki ambayo kama ikitoweka katika jamii ni vigumu Watanzania kuendelea kuimba wimbo wa gloria na unaoitangaza amani wakati mioyo yao imejaa simanzi.
Alisema msingi mkuu wa ujumbe wa wimbo wa Krismasi wa Gloria (utukufu) na pax (amani) umetikiswa na matumaini ya watu wengi yametoweka, hivyo ni jukumu la wananchi kuomba, kusema na kutenda na walio katika nafasi na mamlaka kujihoji na kuchukua hatua kuhusiana na changamoto zilizoelezwa.
Kwa mujibu wa Askofu Mwamakula, usalama kwa maisha ya watu na mali zao umezorota kwa kiasi kikubwa, ukichochewa na vitendo vya utekaji na mauaji vilivyoiweka jamii katika taharuki ikishuhudia watu kadhaa wakiuawa na watu wasiojulikana na wengine kutekwa miezi sita iliyopita.
Alisema pia hali ya usalama wa majengo inaogopesha kwani jamii imeshuhudia baadhi yake yakiungua moto na mengine kuporomoka na kusababisha vifo na majeruhi kutokana na uwezo wa uokozi kuwa mdogo.
“ Bidhaa bandia zinatishia hali ya afya huku kukiwa na hofu ya uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wake madukani, ” alisema
Alisema ukosefu wa ajira umesababisha vijana wengi waliohitimu katika shule, vyuo vikuu kujiingiza katika uhalifu wa aina mbalimbali ikiwamo wa mtandaoni na wale waliofuzu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) bila kupatiwa ajira wanatumiwa na watu wenye nguvu, pesa, mali na mamlaka katika vitendo vya utekaji.
Hali hiyo, alisema huchochea baadhi ya vijana kuingia katika mitego ya kurubuniwa kwa fedha kidogo na kutumika katika vikosi vya ugaidi duniani hasa katika nchi jirani.
Kwa mujibu wa Mwamakula uhalifu wa kisiasa unaonekana ukihalalishwa na watu wenye mamlaka kiasi cha kupelekea hata kufanyika kwa mauaji wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba, mwaka huu. Mambo hayo yakiwakatisha tamaa vijana walioamini kuwa wanaweza kuchagua viongozi ambao wangekuwa wasemaji wao.
Alisema gharama za maisha zimepanda kutokana na kupaa bei za bidhaa huku kipato kikiwa hakijaongezeka, gharama za matibabu zikiwa juu kiasi cha wananchi wa kawaida wakishindwa kuzimudu wakati viongozi na matajiri wakienda nje ya nchi kupata matibabu ya uhakika.
Alisema hali ya ubora wa elimu kwa shule za serikali iko chini kiasi ambacho hakuna hata kiongozi wa serikali anayeweza kuwapeleka watoto au wajukuu zake kusoma katika shule hizo.
Alisema kutokana na hali hiyo, watu wengi wamejengewa matumaini hewa na wanasiasa na viongozi wa dini. Kutokana na shida zilizokithiri, waumini wengi wamekuwa mateka wa viongozi wa dini wenye tamaa ya kuvuna pesa kutoka kwao kwa njia ya njia za ulaghai huku watawala wakitoa ahadi nyingi hewa za kuboresha maisha huku hali ya maisha ikizidi kuzorota.
“Unafiki utajengeka katika nyumba zetu za ibada, vyama vya siasa, katika serikali na jamii yote kwa ujumla. Hivyo, ni wajibu wetu sote kuanza kujihoji na kutafuta majawabu ya maswali yanayoikabili jamii yetu,” alisema.
Alisema katika mazingira hayo, umma wa Watanzania unaingia kusherekea Krismasi ya mwaka 2024 ukiimba ujumbe wa wimbo wa gloria bila kufahamu ni kwa namna gani Yesu anaweza kuwatoa katika changamoto za kimaisha wanazopitia sasa.
“Inawezekana uchechemuzi ambao Yesu aliufanya wakati wa huduma yake ilikuwa ni sehemu ya ukombozi. Yeye alikemea sheria na mifumo kandamizi sambamba na tamaduni zilizokuwa zinawatia watu umaskini ikiwemo ya kutokutenda mambo mema siku ya Sabato,” alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED