MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Dk. Careen-Rose Rwakatale, amewataka viongozi wa CCM katika wilaya mbalimbali za mkoa huo kuhakikisha wanajitoa kikamilifu katika ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama ili kuepuka kudhalilika kwa kufukuzwa kwenye nyumba za kupanga.
3Dk. Rwakatale alitoa kauli hiyo jana wakati akikabidhi bati 50 zenye thamani ya Shilingi milioni 1.5 kwa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero. Bati hizo ni sehemu ya ahadi aliyotoa mwaka 2023 wakati ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya hiyo ulipoanza.
Alisema watumishi wa chama wamekuwa wakikumbwa na changamoto kubwa kwa sababu ya kuishi kwenye nyumba za kupanga, ambapo wakati mwingine wamiliki wa nyumba huweza kuwafukuza au kuwatolea vyombo nje pale wanaposhindwa kulipa kodi, jambo ambalo si tu linawadhalilisha binafsi bali pia linakidhalilisha chama.
“Nyumba za kupanga kwa mtumishi si nzuri. Anaweza kudhalilishwa yeye au chama, hasa pale anapokosa hela ya pango. Lakini akiwa kwenye nyumba ya chama, atakaa kwa utulivu na kutekeleza majukumu yake bila wasiwasi wa kufukuzwa,” alisema Dk. Rwakatale.
Aidha, alieleza kuwa tayari amefanya ziara kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo kuhamasisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama, ambapo ameshachangia ujenzi katika wilaya za Gairo, Morogoro Vijijini, Malinyi na Kilombero. Aliahidi kurejea tena katika maeneo hayo ili kufuatilia maendeleo ya ujenzi na kuendelea kutoa mchango wake kwa maendeleo ya chama.
Dk. Rwakatale aliwaomba pia viongozi wengine wa jumuiya zote tatu za CCM—Wazazi, Umoja wa Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM)—kuendelea kuchangia kwa hali na mali kuhakikisha miradi ya ujenzi inakamilika kwa wakati.
Alifafanua kuwa tangu kuanza kwa ujenzi wa nyumba hiyo ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero, amekuwa sehemu ya mradi huo kwa kutoa mchango wa mwanzo uliowezesha ujenzi kuanza, na hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 80.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero, Saidi Mrisho, alisema ujenzi wa nyumba hiyo yenye vyumba vitatu—ikiwemo chumba chenye choo ndani, choo cha nje, jiko, sebule na stoo—ulianza Desemba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025. Mrisho alisema tayari zaidi ya Shilingi milioni 14 zimetumika, huku kiasi kinachohitajika kukamilisha ujenzi huo kikiwa ni Shilingi milioni 20.
Alisema kukamilika kwa nyumba hiyo kutamsaidia Katibu wa Jumuiya hiyo kuwa karibu na ofisi za chama na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Hivi sasa Katibu huyo anaishi mbali na ofisi za chama, hali inayozidisha changamoto hasa wakati wa mvua nyingi ambapo eneo hilo hujaa maji na kumfanya kushindwa kufika ofisini kwa wakati, au kushindwa kufika kabisa.
Mrisho alitoa pongezi kwa Dk. Rwakatale kwa michango yake ya mara kwa mara na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa chama unakamilika, akimtaka kuendeleza moyo huo hata kwa jumuiya nyingine katika Mkoa wa Morogoro.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero, Jitihadi Jalala Jitihadi, alisema kukamilika kwa nyumba hiyo kutamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kwani kwa sasa hukumbwa na changamoto ya kutofika ofisini kwa wakati kutokana na umbali wa anakoishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Kilombero, Luth-Better Makoloweka, alisema ujenzi wa nyumba hiyo unakwenda sambamba na ujenzi wa nyumba za watumishi wengine wa jumuiya wilayani humo. Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha ulinzi kwa watumishi na kuwaepusha na changamoto mbalimbali za kiusalama, hasa wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED