Tanzania, Angola zakubaliana kuimarisha uchumi, usalama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:45 AM Apr 09 2025
Tanzania, Angola zakubaliana kuimarisha uchumi, usalama
Picha: Mpigapicha Wetu
Tanzania, Angola zakubaliana kuimarisha uchumi, usalama

TANZANIA na Angola zimetia saini hati za makubaliano zinazolenga kudumisha sekta uchumi, na mambo ya kiusalama yenye kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yatakayofungua fursa za biashara za uwekezaji na kuimarisha ulinzi na usalama yametiwa saini na mawaziri wa Ulinzi Tanzania, Dk. Stagomena Tax na Waziri wa Ulinzi wa Angola,  Ernesto Liberdade kwa niaba ya marais wao.

Makubaliano yameingiwa wakati Rais Samia akiwa katika ziara ya siku tatu Luanda, nchini Angola yanayodumisha ushirikiano wa kihistoria uliowekwa na waasisi wa nchi hizo mbili, Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Angola, Hayati Antonio Agustino Neto. 

Wakizingumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya faragha, Ikulu ya Luanda, Rais Samia Suluhu Hassan, amesema  wamekubaliana mambo kadhaa yakiwamo ya hali ya kisiasa na uchumi wa nchi zao.

Amesema Tanzania ina nia ya kuimarisha ushirikiano wao, ili kuondoa hofu katika maendeleo ya kiuchumi.

Kadhalika alitangaza kuondoa Visa kwa watalii wanaotoka nchini Angola, kufika Tanzania na kuwakaribisha wafanyabiashara wa nchi hiyo kutembelea Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC), ili kujionea fursa za uwekezaji kwenye madini na kutoa fursa za ajira kwa vijana.

Ametaja fursa nyingine kuwa ni kwenye kilimo, utalii na uchumi wa buluu. 

Rais Samia pia amemwalika Rais Lorenco kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi ya maonesho ya kimataifa ya kibiashara, maarufu Sabasaba, Julai, mwaka huu.

Ameliomba Taifa la Angola kuiunga mkono Tanzania kwenye nafasi inayogombaniwa ya Ukurugenzi kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo Tanzania inawakilishwa mgombea wake Profesa Mohamed Janabi.

Akizumgumza katika mkutano huo, Rais wa Angola, Joao Manual Lorenco, amesema anaishukuru Tanzania kwa kujitoa kuisidia nchi yao ilipokuwa kwenye harakati za ukombozi kwa kuwafadhili raia wake kwa kuwapa makazi, mahitaji mengine na usalama.

Amesema historia iliyowekwa na Hayati Nyerere kwenye nchi yao, imewafanya kumpa heshima ya kumpa jina la hospitali kubwa nchini humo itakayozinduliwa 1Novemba, mwaka huu, wakati nchi hiyo inaposherehekea miaka 50 ya uhuru wake na wamempa heshima Rais Samia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wake.

Aidha, ameahidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili na bara zima la Afrika.

Awali, katika ziara hiyo Rais Samia ametembelea mnara wa Mashujaa wa Angola na kuweka shada la maua na alihutubia Bunge la nchi hiyo akiwa Rais wa kwanza mwanamke kilihutibia.