CHADEMA yapewa siku 21 kesi kuhusu mali za chama

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 06:43 PM Apr 17 2025
news
CHADEMA
Jengo la CHADEMA Makao Makuu Mkocheni, Dar es Salaam

MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekiamuru Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndani ya siku 21 kiwe kiwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi katika kesi ya mgawanyo wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Kesi hiyo imefunguliwa na wanachama wa chama hicho dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA (mdaiwa wa kwanza) na Katibu Mkuu wa CHADEMA, akiwa mdaiwa wa pili.

Amri hiyo imetolewa leo Aprili 18,2025 na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama hiyo wakati kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilipotajwa kwa mara ya kwanza, baada ya mawakili wa CHADEMA, Jeston Justine na John Chogomo kuomba wapatiwe muda huo wa kuandaa na kuwasilisha utetezi wao.

Hata hivyo, Wakili wa wadai Shaban Marijani hakupinga ombi hilo la CHADEMA ndipo Jaji Mwanga akaridhia na kutoa siku hizo ambapo wanatakiwa kuwasilisha utetezi kabla ya Mei 21, 2025 mahakamani hapo.

"Maombi yamekubaliwa mnapewa siku 21 kuanzia leo (jana) kuwasilisha utetezi wake. Mnatakiwa kuwasilisha mahakamani utetezi wenu kabla ya Mei 21, 2025", amesema Jaji Mwanga.

Jaji Mwanga amesema kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 12,2025 kwa ajili ya kuangalia kama Chadema watakuwa wametekeleza kilichotolewa na Mahakama.

Kesi hiyo  imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye anajitambulisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa  chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajotambulisha la wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho.

Wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru kwamba wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.

Wamedai kuwa wameomba Mahakama itamke hivyo, kwa sababu kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia.

Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Pia, wanaomba mahakama isitishe kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya mahakama, pia itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.