Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema kuwa kuanzishwa kwa bustani za wanyama katika vikosi vya JKT ni hatua mahsusi ya kuongeza vyanzo vya mapato ya vikosi, kutangaza utalii wa ndani, pamoja na kuwa sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba za kulala wageni katika bustani ya wanyama inayosimamiwa na Kikosi cha Jeshi 832 Ruvu JKT, Meja Jenerali Mabele alisema mradi huo ni wa kipekee na una mchango mkubwa kwa Taifa.
“Bustani hii si tu inatangaza utalii, bali pia inasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kufika mbuga kama Mikumi, kuwa na nafasi ya kuwaona wanyama kwa ukaribu zaidi,” alisema Meja Jenerali Mabele.
Aliongeza kuwa bustani kama hiyo tayari imeanzishwa pia katika Kikosi cha Mbweni jijini Dar es Salaam, na kuna mpango wa kuongeza idadi ya wanyama rafiki katika maeneo hayo ili kuwavutia zaidi watalii wa ndani na nje ya nchi.
Amesema ujenzi wa nyumba hizo za kulala wageni utakuwa chachu ya kukuza utalii wa ndani, kwani wageni watakaotembelea bustani hiyo sasa wataweza kufurahia mazingira kwa utulivu na huduma kamili mahali hapo.
Katika hafla hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Ruvu JKT, Kanali Peter Mnyani, alisema vijana wanaopitia mafunzo katika kikosi hicho wamekuwa wakinufaika na mafunzo ya uzalendo sambamba na kujifunza shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kilimo na utalii.
Mbali na tukio hilo, Meja Jenerali Mabele pia alifunga rasmi mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea chini ya Operesheni Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, yaliyofanyika katika Kikosi cha 832 Ruvu JKT.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED