Makalla:Hoja ya Heche ya bandari, makaa ya mawe ni dhaifu

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:52 AM Apr 18 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amesema hoja ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bara, John Heche, kuhusu makaa ya mawe na uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam ni dhaifu.

Amemtaka asidandie masuala ya  kiuchumi kwa kuwa hana elimu hiyo wala uzoefu.

Amesema jana (juzi) alimsikia Heche, akizungumzia makaa ya mawe kwamba yanabebwa malori kwa malori kwenda nje ya nchi huku vijana wakibaki na mashimo.

Akimjibu katika mkutano wa hadhara uliofanyika Masasi Mjini, wakati akihitimisha ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Makalla amesema Heche hana elimu wala uzoefu wa masuala ya uchumi.

“Jana, (juzi)  nilimsikia John Heche, akizungumzia makaa ya mawe yanabebwa malori kwa malori kwenda nje huku vijana wakibaki na mashimo.“Heche anasema tumeshindwa kuendesha bandari, ninataka nimwaambie Heche asidandie hoja za uchumi hana elimu wala uzoefu. Atuulize sisi wenye CPA,  mimi ni mwenezi lakini naweza kusema mambo ya uchumi.“Makaa ya mawe ni fursa, makaa ya mawe eti yanachimbwa yanabaki mashimo sasa alitaka makaa ya mawe tuyafanyie nini,” anasema.

Kadhalika amesema Bandari ya Dar es Salaam na ya Mtwara yamefanyika maboresho makubwa akimweleza kuwa kumweka mtu wa kuiendesha hilo si kosa.