Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), wamesema bado jamii ya watu wenye mahitaji maalum nchini, wanakabiliwa na changamoto ya ushindani sawa katika fursa mbalimbali, ikiwamo ajira.
Mwanafunzi wa stashahada ya usimamizi wa ushirika na uhasibu wa chuo hicho, Josephine Mndolwa, amesema kukosekana kwa hali ya usawa kunawafanya wenye mahitaji maalum kushindwa kupata mahitaji maalum na hivyo kuendelea kuwa kundi lililoachwa nyuma zaidi kiuchumi.
Alikuwa akizungumza katika semina elekezi ya kuwajengea uwezo pamoja na kula pamoja na jamii hiyo ya wenye mahitaji maalum kutoka MoCU, Shule ya Sekondari Old Moshi, Shule ya Msingi Mwereni, Shule ya Msingi Rau, Chuo Kikuu cha Tiba KCMC, Chuo cha Usimamizi wa Wanyapori Mweka, Sekondari ya Ufundi Moshi na Chuo Kikuu cha Kikatolili Mwenge.
Kuhusu ukatili wa kukatwa na kuchukuliwa viungo vya watu wenye ulemavu, jamii hiyo imeeleza kuwa bado upo na ni tishio katika jamii.
Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Gabriella Rehabilitation Centre, Nimwindael Mdee, akizungumza na jamii hiyo amesema: "Natambua kuwa channgamoto za wanafunzi wenye mahitaji maalum shuleni, vyuoni na hasa MoCU bado zipo; hasa ukizingatia uhaba wa rasilimali fedha na vifaa uliopo. Ni wazi kuwa vifaa saidizi vonavyotolewa na serikali havitoshelezi mahitaji."
Mdee, amesema ametoa rai kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kutambua kuwa wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wa maendeleo kwa jumuiya ya MoCU, familia zao, jamii ya kitanzania na dunia kwa ujumla.
Akiwasilisha mada juu ya kujitambua uthamani wao na uthubutu, Meneja Programu wa Shirika la Tusonge CDO, Lawi Msemwa, amesema watu bilioni moja duniani wanatokana na watu wenye ulemavu.
"Kati ya hao, asilimia 80 ya watu hao wenye mahitaji maalum wanapatikana Afrika. Lakini pia kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, nchini Tanzania watu wenye ulemavu wako zaidi ya milioni tatu."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED