UONGOZI wa Chama cha Mchezo wa Wushu Tanzania (TWA), umesema unaendelea na maandalizi kuelekea kwenye mashindano yatakayoanza Juni 14 hadi 15, mwaka huu, nchini Rwanda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mei 12, 2025, Katibu Mkuu wa chama hicho, Sempai Kapipi, amesema maandalizi kuelekea kwenye mashindano hayo yanaendelea vema.
"Wachezaji wetu kwa sasa wanafanya mazoezi ya pamoja, kwa ajili ya kuimarisha miili yao wakiwa na malengo ya kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo,” amesema Kapipi.
Amesema katika mashindano hayo watashindana michezo mbalimbali, ukiwamo kupigana pamoja na ule wa kutumia silaha za aina zote.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuunganisha umoja kati ya Tanzania pamoja na nchi ya Rwanda, ambayo hufanyika kila mwaka.
"Kwa upande wetu tutapeleka wachezaji 10 pamoja na viongozi wawili tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutuunga mkono, ili kutimiza malengo yetu,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED