Ningependa tutafakari kwa pamoja uwezekano wa kuwa na siku zijazo zilizo bora kabisa katika uhusiano kati ya Marekani na Tanzania ambapo tutakuwa tumejenga ustawi mkubwa sana kwa mataifa yetu yote mawili. Katika siku hizo njema zijazo, safari za ndege za moja kwa moja zitaiunganisha Marekani na Tanzania, zikisafirisha mamia ya maelfu ya watalii wa Kimarekani kila mwaka kuja kufurahia hifadhi za wanyamapori, fukwe na hoteli za Tanzania.
Makampuni makubwa ya Kimarekani yatakuwa yanawekeza mabilioni katika sekta za madini, utalii na sekta nyinginezo hapa Tanzania, yakizalisha nafasi nyingi za ajira na utajiri kwa Wamarekani na Watanzania.
Majeshi yetu yanashirikiana kudumisha utulivu wa kikanda na kulinda njia na bandari za kibiashara katika Bahari ya Hindi, kuhakikisha njia salama, pana na anuai za ugavi kwa uchumi wa dunia. Wanasayansi wetu na wataalamu wa afya ya dunia wanashirikiana kufanya utafiti ili kulinda mataifa yetu na dunia nzima dhidi ya janga kubwa lijalo la kiafya. Bidhaa, huduma, na uwekezaji kutoka Marekani vinaingia Tanzania bila vikwazo visivyo wazi au visivyo vya haki. Mustakabali huu ni wenye matumaini, sivyo? Uliojaa fursa.
Tunaweza kuanza kuujenga mustakabali huu sasa. Marekani imewekeza mabilioni ya dola katika miongo iliyopita kwenye sekta za afya, elimu, na kilimo nchini Tanzania, ikiokoa maisha na na kuboresha riziki. Ni wakati sasa wa kuthibitisha uimara wa uwekezaji huu, na kwa Tanzania, kama nchi ya kipato cha kati yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kuingia katika hatua mpya ya ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi. Marekani inafurahi kufungua ukurasa huu mpya pamoja na ninyi - kusonga mbele kwa pamoja katika enzi mpya ya ushirikiano, ambapo biashara na uwekezaji ndio vinakuwa kipaumbele katika uhusiano rasmi kati ya Marekani na Tanzania unaozinufaisha pande zote mbili.
Marekani inataka ushirikiano uliojikita katika fursa za pamoja za kiuchumi. Kuna makampuni ya Kimarekani yaliyo tayari kuwekeza katika fursa zinazowanufaisha Wamarekani na Watanzania zitakazounda ajira zenye thamani kubwa kwa pande zote mbili. Makampuni haya yako tayari kushirikiana katika uwekezaji utakaoiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na rasilimali zake za madini na nishati; kupanua upatikanaji wa mtandao wa intaneti nchi nzima; kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo ili kuongeza kuijumuisha kikamilifu Tanzania katika minyororo ya ugavi na usambazaji ya kimataifa; na kuongeza tija ya wakulima. Hata hivyo, Sehemu kubwa ya uwekezaji huu umekwama kutokana na majadiliano yaliyokwama au yanayochukua muda mrefu kupindukia, masharti magumu ya kodi yanayokinzana na vivutio vya uwekezaji vilivyoahidiwa, na vikwazo vingine visivyo vya kibiashara. Tukiondoa vikwazo hivi na kukamilisha mikataba, tutazalisha simulizi nzuri zitakazovutia wawekezaji wengi zaidi kuja Tanzania. Mafanikio huzaa mafanikio.
Uchaguzi huru na wa haki uliofanyika kwa amani, ambapo Watanzania wana nafasi ya kusikika kwa kuchagua mustakabali wao, ni muhimu kwa mafanikio yetu ya pamoja katika kuharakisha ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi, kupambana na rushwa na kuimarisha mifumo ya ndani, pamoja na kupanua biashara na uwekezaji wa pande mbili unaowanufaisha wananchi wote.
Kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rubio alivyoeleza mara kadhaa, “Marekani kwanza haimaanishi Marekani peke yake.” Ili Marekani ifanikishe malengo yake, lazima tushirikiane na nchi washirika kama Tanzania kufungua fursa za kiuchumi, kushirikiana kwenye vipaumbele vya kiusalama, na kufanikisha ukuaji. Mustakabali huu wa uhusiano kati ya Marekani na Tanzania uko karibu kuliko tunavyodhani. Kuufikia kunahitaji dhamira ya kisiasa kutoka kwa nchi zetu zote mbili na kujitolea kwa dhati kujenga ushirikiano wa kweli. Ustawi zaidi, usalama zaidi. Marekani iko tayari kufanikisha haya kwa pamoja. Je, Tanzania iko tayari?
Na Kaimu Balozi wa Marekani Andrew Lentz
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED