KIKOSI cha Simba kinatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kuelekea nchini Morocco, kwa ajili ya mchezo wao wa Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane, utakaochezwa Mei 17, mwaka huu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally, amesema Mkuu wa msafara wao huo anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, pamoja na wachezaji 24 na kudai idadi ya mashabiki watakaosafiri nao wanatarajia kuwatangaza kabla ya safari.
"Tutaondoka kesho alfajiri, kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wetu huo, tukiwa na malengo ya kushinda mchezo huo, wenye kauli mbiu Tunabeba," amesema Ally.
Meneja huyo amesema mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani kutokana na rekodi ya mpinzani wanayekwenda kukutana Naye, kwani alishacheza fainali mara nne pamoja na kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo.
Amesema licha ya mchezo huo kuwa mgumu watapambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wakiwa ugenini pamoja na ule watakaoucheza Mei 25, mwaka huu, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Amesema hali ya wachezaji inaendelea vizuri kwani saikolojia zao zipo juu na kusema kila shabiki ambaye anahitaji kusafiri anapaswa kulipa dola 1,200 ambazo zitawasaidia siku zote watakazokuwa nchini humo, ikiwamo malazi, usafiri pamoja na bima ya afya ambayo kila mmoja anatakiwa kwenda nayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED