TMA yatoa tahadhari magonjwa kipindi cha kipupwe

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 05:12 PM May 22 2025
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a.
Picha: Faustine Feliciane
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi katika baadhi ya mikoa nchini kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yanayochochewa na hali ya baridi na vumbi, yakiwemo homa ya mapafu, magonjwa ya macho na yale ya mifugo, kutokana na hali ya kipupwe inayotarajiwa kuanzia Juni hadi Agosti 2025.

Tahadhari hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, alipokuwa akielezea mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha kipupwe kwa mwaka huu.

Dk. Chang’a amesema, kipindi hiki kinatarajiwa kuongozwa na upepo wa wastani kutoka Kusini Mashariki katika maeneo mengi ya nchi, pamoja na vipindi vichache vya upepo mkali kutoka Kusini (upepo wa kusi), hasa katika miezi ya Juni na Julai kwa maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na nchi kavu.

Ameeleza kuwa hali ya baridi ya wastani hadi kali inatarajiwa kutokea katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa Mkoa wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Dk. Chang’a, maeneo ya mwambao wa Pwani ya Kaskazini ikijumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga, yanatarajiwa kuwa na joto la chini, huku maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba yakitarajiwa kupata nyuzi joto kati ya 16 hadi 24.

“Katika maeneo haya yenye baridi na upepo, tunatoa rai kwa wananchi kujikinga na magonjwa kama homa ya mapafu na macho, sambamba na wafugaji kuwa makini ili kuepusha magonjwa kwa mifugo yao,” amesema Dk. Chang’a.

Ameongeza kuwa katika maeneo ya miinuko, joto la chini linatarajiwa kufikia nyuzi joto 12. Kwa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki – mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara – joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 hadi 20.

Kadhalika, Kanda ya Ziwa – mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu – inatarajiwa kuwa na joto la chini kati ya nyuzi joto 10 hadi 18.

“Katika upande wa Magharibi wa nchi yetu – mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma – joto la chini linatarajiwa kufikia nyuzi joto 10. Kwa Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Singida na Dodoma, kiwango cha joto kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 hadi 20,” ameongeza.

Kwa Nyanda za Juu Kusini Magharibi – mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe – pamoja na maeneo ya Kusini mwa Mkoa wa Morogoro, joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 6 hadi 20, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kushuka chini ya nyuzi joto 6.

Kwa upande wa Kanda ya Kusini – mikoa ya Mtwara na Lindi – joto la chini linatarajiwa kushuka chini ya nyuzi joto 12.