Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kichama Kahama, Kasigwa Adram, leo Mei 22, 2025, amechukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Msalala, akiahidi kumuondoa mbunge wa sasa kupitia vipaumbele vitatu vinavyogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika uzinduzi wa zoezi la uchukuaji wa fomu za ubunge na udiwani ndani ya chama, Kasigwa alisema vipaumbele vyake ni Afya, Kilimo, Elimu ya Sayansi na TEHAMA pamoja na Utawala Bora.
“Nitahakikisha wananchi wanapata bima za afya, tunapunguza vifo vya wajawazito na watoto, tunaleta ruzuku ya pembejeo, masoko ya uhakika, na tunasimamia elimu bora ya sayansi na TEHAMA, sambamba na kudumisha utawala bora kwa maendeleo ya watu wetu,” amesema Kasigwa.
Zoezi hilo la uchukuaji wa fomu limezinduliwa leo na linatarajiwa kukamilika Mei 30, 2025, ambapo chama kimeweka wazi kuwa mwanachama yeyote atakayebainika kutoa au kupokea rushwa ili kupitishwa, ataondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi.
Kwa upande wake, Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Kahama, Benedict Shija, amesema chama kimejipanga kusimamisha wagombea kwa asilimia 100 katika nafasi za urais, ubunge na udiwani nchi nzima.
“Sifa za kugombea ni kuwa na umri wa kuanzia miaka 21 kwa ubunge na udiwani, na miaka 41 kwa nafasi ya urais. Fomu ya udiwani ni Sh. 30,000, ubunge na viti maalum ni Sh. 100,000, na fomu ya urais ni Sh. 1,000,000,” amesema Shija.
Aidha, amewaonya wanachama dhidi ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kumvumilia mgombea mwenye tabia ya kutumia pesa au ushawishi haramu kupata nafasi za uongozi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED