Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini katika kuhakikisha wanazidisha uangalizi wa mtoto mwenye umri 0-8 upande wa afya, lishe, ulinzi na ujifunzaji wa awali.
Mtanda alitoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa nusu Mwaka wa tathmini ya utekelezaji wa program jumuishi ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (MMMAM) kuelekea kilele cha maadhimisha siku ya kimataifa ya familia iliyopewa jina la ‘Tanzania Malezi Summit’ na kauli mbiu isemayo ‘Mtoto ni Malezi’.
Amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa zaidi ya robo ya Watanzania ni watoto wenye umri wa kati ya miaka 0 hadi 8 na kueleza kuwa ipo haja ya kuwekeza kwa makundi hayo mapema kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vizazi vijavyo.
“Asilimia 47 ya watoto wa miezi 24 hadi 59 wanaonesha dalili za ukuaji timilifu wa kiafya na kihisia, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendeleza juhudi katika sekta ya afya, lishe, ulinzi na ujifunzaji wa awali,” amesema Mtanda.
Amesema taifa haliwezi kuzungumzia kuhusu Maendeleo kama jamii haizungumzii kuhusu watoto ambao wamejengwa katika misingi imara ya kimalezi na makuzi yenye tija.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Sebastian Kitiku alisema kwa Watoto wenye umri 0-8 wakiwekeza vya kutosha matokeo yake ni makubwa sana.
“Unatakiwa kufanya mambo machache kwa kuwekeza vya kutosha na kumfanya mtoto kuwa na uelewa mkubwa darasani, uwezo mkubwa wa kupambanua mambo na kuchagua mambo katika umri wake mdogo na ataendelea mpaka Maisha yake yote na hili litatusaidia kuwa na Taifa lenye vizazi bora,”amesema Kitiku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED